Hukumu ya Tido mpaka mwakani

19Dec 2018
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Hukumu ya Tido mpaka mwakani

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imesema hukumu ya kesi inayomkabili Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando, haijawa tayari hivyo itasomwa Januari 25, mwakani.

Tido anakabiliwa na tuhuma za  matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh. milioni 887.1.

Kesi hiyo ilipangwa kusomwa hukumu jana na  Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, lakini alisema bado haijawa tayari.

"Hukumu bado haijawa tayari nitaisoma Januari 25, 2019. Dhamana ya mshtakiwa inaendelea," alisema Hakimu Shaidi.

Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Nassoro Katuga na Patrick Mwita na Leonard Swai, ulidai kuwa kesi imepangwa kwa ajili ya hukumu na wako tayari.

Hakimu alisema hukumu bado haijawa tayari na kwamba itasomwa tarehe iliyopangwa. Wakili wa utetezi, Dk. Ramadhani Maleta, alidai kuwa upande wa utetezi hauna pingamizi.

Oktoba 30, mwaka huu, upande wa utetezi ukiongozwa na mawakili (kwa sasa marehemu) Martin Matunda na Dk. Maleta walifunga ushahidi wa upande wao. Upande wa Jamhuri uliita mashahidi  wanne dhidi ya Tido.

Miongoni mwa  mashahidi  wa upande wa mashtaka waliotoa ushahidi  katika kesi hiyo ni pamoja na  Ofisa Uchunguzi wa Takukuru, Victor Lesuya; Mwanasheria wa TBC, Gwakisa Mlawa na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa TBC, Clement Mshana.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Juni 16, 2008,   akiwa  Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Tido wakati huo akiwa mkurugenzi mkuu wa TBC, kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kutia saini mkataba wa kuendesha na kutangaza vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume cha Sheria ya Ununuzi wa Umma na kuinufaisha BVl.

Katika shtaka la pili, Tido anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20, 2008 alipotia saini makubaliano kwa utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVl.

Katika shtaka la tatu, anadaiwa Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.

Katika shtaka la nne, anadaiwa kuwa  Novemba 16, 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kwa kutia saini mkataba wa makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.

Katika shtaka la mwisho,  anadaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008 akiwa UAE, Tido aliisababishia TBC hasara ya Sh.887,122,219.19.