Hukumu za Tanzania ujangili zapewa tano

25Jun 2019
Salome Kitomari
Nipashe
Hukumu za Tanzania ujangili zapewa tano

TANZANIA inatajwa kuwa iko vizuri kwenye kuhukumu wanaokutwa na hatia ya kuhusika na ujangili wa maliasili na wanyamapori.

Mwanasheria wa Shirika la Kudhibiti Usafirishaji Haramu wa Wanyamapori Tanzania (Traffic), Linah Clifford.

Akizungumza hivi karibuni na Nipashe, Mwanasheria wa Shirika la Kudhibiti Usafirishaji Haramu wa Wanyamapori Tanzania (Traffic), Linah Clifford, alisema ushirikiano wa vyombo vyote vya dola na nia ya kupambana na ujangili kumeiweka Tanzania pazuri.

Alisema kwa nchi za Afrika, Tanzania inaongoza kwa kutoa hukumu ya muda mrefu kama mtu kuhukumiwa miaka 20 au zaidi.

“Tanzania inatajwa kuwa inachukulia kwa uzito na umakini makosa ya wanyamapori maana wapo ambao wamehukumiwa miaka 20 au 30 na wengine ikiunganishwa inafika 50,” alisema Clifford.

Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, Tanzania ukikutwa na nyara ya serikali kama nyama, ngozi au meno ya wanyamapori, linachukuliwa kwa uzito na vyombo vyote vinashirikiana.

Alisema nchi nyingine kama Malawi, Msumbiji na Uganda zina sheria nzuri, lakini zina hukumu miaka mitano au 10.

“Watuhumiwa wengi wanakimbilia kwenye nchi hizo kuliko akikamatiwe Tanzania bora akakamatiwe au kutenda kosa kwingine kwa kuwa sheria zetu zina meno ya kutosha,” alisema.

Aidha, alisema wana miradi zaidi ya 100 ya kupambana na ujangili wa wanyamapori, ikiwamo kutoa mafunzo kwa mahakimu na waendesha mashtaka jinsi ya kuona umuhimu wa kesi za wanyamapori na maliasili.

“Tunafanya utafiti kuwajua kwamba kwanini watu wanafanya biashara ya wanyamapori kama ni kwa ajili ya chakula, dawa au biashara tunafanyakazi na sekta za biashara kwenye eneo la usafirishaji kujua kinachotakiwa kama mtu anasafirisha,” aliongeza.

Alisema kwa kushirikiana na vyombo mbalimbali, wameweka mbwa wenye utaalamu wa kutambua nyara za serikali kwenye viwanja vya ndege na bandari pamoja na utafiti kwenye eneo la uvuvi kwenye mikoa inayozungukwa na ziwa na bahari.

Alisema lengo ni kudhibiti biashara haramu ya nyara za serikali na kwa ushirikiano wa sekta mbalimbali wamefanikiwa kumaliza biashara ya meno ya tembo na pembe za faru.

Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, wametengeneza teknolojia ya kukagua magari kwenye vituo mbalimbali kwa kujua kinachoingia na kutoka nchini.

000000

Habari Kubwa