IAA, NIC yazindua mtaala mpya elimu ya bima

28Jul 2021
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
IAA, NIC yazindua mtaala mpya elimu ya bima

CHUO cha Uhasibu Arusha (IAA) kwa kushirikiana na Shirika la Taifa la Bima (NIC), kimezindua mtaala mpya wa elimu ya bima na viashiria hatarishi, utakaosaidia wanafunzi kupata uzoefu wa kazi wakiwa masomoni.

Mkurugenzi IAA, Profesa Eliamani Sedoyeka.

Mtaala huo unaelekeza mwanafunzi kusoma darasani kwa miezi 18 na kujifunza kwa vitendo kazini kwa miezi 14 katika kipindi cha miaka mitatu ya masomo yao ya shahada.

Mkurugenzi IAA, Profesa Eliamani Sedoyeka, aliyasema hayo mkoani Dar es Salaam, wakati akizundua mtaala huo unaolenga kuongeza ustadi kwa wahitimu na kupanua nafasi ajira kwa wahitimu wa masomo hayo.

Amesema mtaala huo utawawezesha wahitimu pia kujiajiri kwa kufungua kampuni zitakazosaidia kuajiri vijana wengine zaidi.

“Kupitia mtaala huu, tunatoa uwezeshaji kwa vijana wahitimu ambao wanataka kujiajiri kufikia malengo yao ili kusaidia kukuza uchumi wao na taifa kwa ujumla,” amesema Prof. Sedoyeko.

Alisema katika kuuandaa mtaala huo, walishirikiana na Wizara ya Fedha na Shirika la Kazi Duniani (ILO), ili kupata vigezo zinavyoweza kuzalisha wahitimu wanaokidhi vigezo.

Naye Mkurugenzi wa NIC, Dk. Elirehema Doriye, amesema ushirikiano huo utawasaidia wanafunzi wanaoenda kufanya masomo kwa vitendo katika ofisi zao, kujifunza kama watumishi na siyo kama wanafunzi.

Amesema wahitimu wengi wanakosa sifa za kuajirika kwa sababu ya kushindwa kuendana na tamaduni za ofisi wanazoenda kuomba kazi hivyo watahakikisha wanafunzi hao wanakidhi vigezo vyote.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) Jane Nyimbo, alikitaka chuo hicho, kuwafuatilia wanafunzi wanaokuwa mafunzoni ili kutimiza lengo hilo kikamilifu.

“Chuo kijipange kuwafuatilia wanafunzi wanafanya nini sehemu za kazi ili wanapomaliza wawe kweli wametimiza vigezo,” amesema Jane.

Naye mgeni rasmi katika tukio hilo, Mkurugenzi wa Usimamizi na Ukaguzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Shughuli za Bima (TIRA), Neema Lutula, amesema, mfumo huo utawasaidia wanafunzi kupata uzoefu na jamii kunufaikana uwepo wa bima katika uchumi na jamii kwa ujumla.

Amesema serikali imejidhatiti kuimarisha sekta ya bima na kwa kiasi kikubwa na imerejesha imani ya wananchi kwa waendelee kubuni mitaala mipya ya kutatua changamoto katoka kwa jamii.

Habari Kubwa