Iddi Simba afariki, kuzikwa leo Kisutu

14Feb 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Iddi Simba afariki, kuzikwa leo Kisutu

MWANASIASA mkongwe na Waziri wa zamani wa Viwanda na Biashara, Iddi Simba, amefariki dunia.

Taarifa iliyosambaa jana katika mitandao ya habari na kuthibitishwa na mtoto wake, Ahmad Simba, ilisema Simba alifariki dunia katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alikokuwa akipatiwa matibabu.

Ahmad alikaririwa akisema familia, ndugu, jamaa na marafiki walikuwa wanakusanyika nyumbani kwa marehemu kwa ajili ya kupanga mipango ya maziko yake.

Hata hivyo, taarifa zilizopatikana jana jioni zilisema mwanasiasa huyo atazikwa leo katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam, baada ya Sala ya Ijumaa.

Iddi Simba, ambaye alizaliwa Oktoba 8, 1935 alipata elimu yake katika vyuo vikuu vya Punjab, Pakistan na Toulouse, Ufaransa, licha ya kuwa mwanasiasa, alianza kazi katika utumishi wa umma na baadaye taasisi za fedha za kimataifa.

Alianza utumishi wa umma akiwa Mkurugenzi wa Mipango Msaidizi katika iliyokuwa Wizara ya Uchumi na Mipango na baadaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji Mbadala wa Benki ya Dunia mwaka 1966 hadi 1968.

Baada ya hapo aliteuliwa kuwa Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki nafasi aliyoishika kwa miaka 10 hadi mwaka 1978. Mwaka 1978 hadi 1980 alikuwa Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Kutokana na kustaafu utumishi katika taasisi hizo, Iddi Simba alijikita kwenye biashara hadi kifo chake, lakini alishika nyadhifa mbalimbali za kisiasa.

Miongoni mwa nyadhifa hizo ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM kuanzia mwaka 1996 hadi 1999 na kwa nafasi hiyo akawa mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC).

Sambamba na nafasi hizo, aliwahi kuwa Mbunge wa Ilala kuanzia mwaka 1995 hadi 2015 na Waziri wa Viwanda na Biashara mwaka 2000 hadi 2002 alipojiuzulu kutokana na kashfa ya vibali vya uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi.

Habari Kubwa