Idris Sultan mikononi mwa polisi

21May 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Idris Sultan mikononi mwa polisi

JESHI la Polisi linamshikilia mchekeshaji Idris Sultan, baada ya kukamatwa tena juzi jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Edward Bukombe, aliliambia Nipashe jana kuwa, Idris alikamatwa na kufikishwa Kituo cha Polisi Oysterbay ingawa kwa wakati huo (jana jioni) alikuwa ameshaondolewa na kupelekwa Makao Makuu ya jeshi hilo kwa mahojiano.

“Aliletwa hapa ingawa kwa sasa hayupo hapa, amepelekwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kwa mahojiano, wao ndiyo wanaweza kusema chochote,” alisema.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime, alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema kwa wakati huo alikuwa jijini Dodoma na kuahidi kufuatilia na alipotafutwa baadaye jioni, simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa.

Mwaka 2014, Idris alishinda tuzo za Big Brother Africa na mwezi Machi mwaka huu alifikishwa katika Mahakama ya Kisutu kwa kuweka maudhui mtandaoni bila leseni.

Habari Kubwa