IGP ataka bima ya maisha kwa askari

30Jul 2021
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
IGP ataka bima ya maisha kwa askari

MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, amesema ni jambo la msingi kwa watumishi wa jeshi hilo kuingia katika bima ya maisha kwa sababu ni kundi ambalo lipo katika hatari ya kupoteza maisha wakati wowote.

IGP Sirro aliyasema hayo jana mkoani Dar es Salaam wakati jeshi hilo lilipotia saini hati ya makubaliano na Shirika la Bima la Taifa (NIC) ili kuwezesha askari na familia zao kujiunga katika bima hiyo.

“Ukiambiwa kuna majambazi wapo benki wenye silaha ukienda pale kuna mawili -- urudi au kutorudi, na hapo hapo tuna familia zetu, vijana wetu kuingia kwenye bima ya maisha ni jambo la msingi,” alisema.

IGP Sirro alisema askari wa usalama barabarani nao wamekuwa wakigongwa na magari.

"Unamsimamisha dereva, unakuta amelewa bangi, haangalii kama ni ofisa polisi, anamgonga. Kwa hiyo, kuwa na bima ya maisha ni jambo la msingi,” alifafanua.

Kiongozi huyo alitaja kundi lingine linalotakiwa kuingia katika utaratibu huo wa bima ya maisha ni vijana wanaoendesha pikipiki, maarufu bodaboda.

Alisema shida ni kwamba kijana ananunua pikipiki asubuhi, anajifunza mchana, jioni anaingia kwenye biashara ya kubeba abiria.

“Lazima tupanue wigo kuhakikisha hawa Watanzania wenzetu ambao ni nguvu ya taifa wanashirikishwa katika hii bima ili kesho na keshokutwa wakiondoka, wanaobaki wasaidiwe,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Dk. Elirehema Doriye, alisema mwelekeo wa shirika hilo kuanzia 2016/17 hadi 2019/20 unaonyesha unaimarika na kuongeza faida.

Alisema hadi kufikia Juni mwaka jana, shirika limeendelea kuimarika kwa kupata faida baada ya kodi ya Sh. bilioni 20.99 kulinganishwa na Sh. bilioni 3.32 kwa mwaka 2018/19.

“Shirika limelipa jumla ya kodi ya Sh. bilioni 11.86 kwa mwaka wa fedha 2019/20 na Sh. bilioni 13.61 kwa mwaka wa fedha 2020/21,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema rasilimali halisi zimeendelea kukua kutoka Sh. bilioni 48.73 kwa mwaka wa fedha 2018/19 mpaka Sh. bilioni 72.16 mwaka 2019/20.