IGP atoa siri ya kupangua makamanda wa polisi

14Feb 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
IGP atoa siri ya kupangua makamanda wa polisi

MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, ametoa siri ya mabadiliko ya makamanda wa polisi wa mikoa ambayo amekuwa akiyafanya mara kwa mara kuwa husababishwa na wahusika kushindwa kutekeleza mambo makubwa matatu kwenye mikoa yao.

MKUU wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, picha mtandao

Akizungumza kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni jana asubuhi, IGP Sirro aliyataja mambo hayo ambayo makamanda wanatakiwa kuyatekeleza kwenye mikoa yao kuwa ni kupambana na uhalifu, nidhamu na kuwa na ushirikiano na wananchi wa mkoa husika.

Akijibu swali lililohoji ninini tafsiri ya mabadiliko ya makamanda wa polisi wa mikoa aliyoyafanya hivi karibuni, IGP Sirro alisema mabadiliko hayo ni ya kawaida na kwamba asili ya kazi zao ni kama timu ya mpira.

“Ninapompeleka kamanda wa polisi mkoa fulani lengo langu ni kwanza kupambana na uhalifu, nidhamu na ushirikiano na wananchi uwe mkubwa kwa sababu pale ananiwakilisha,” alisema na kuongeza:

“Jambo likienda ndivyo sivyo sina njia nyingine kwa sababu utaratibu wetu ni kuambiana sasa utamwambia kesho utamwambia tena na ukiona anakwenda tofauti unamrudisha unapeleka mpiganaji mwingine, kwa hiyo mabadiliko yale ni ya kawaida ili kuongeza ufanisi ndani ya Jeshi la Polisi.”

Alisisitiza kuwa hawezi kupeleka makamanda kwenye mikoa yenye askari wanaojituma, wanaozuia uhalifu na wanaoshirikiana na wananchi.

“Kazi ya polisi haifanyiwi chumbani... ikishaharibika mahali popote utajua tu kwa mfano matukio ya mauaji yaliyotokea Mkoa wa Njombe lazima nijiulize kuna shida gani je, huyo kamanda vipi, kwa nini yametokea,” alisema na kuongeza:

“Ukifuatilia unajua alifanya kwa kadri ya uwezo wake lakini mambo mengine lazima tusaidie, kwa hiyo mabadiliko mengine huwa nayafanya ili kuongeza ufanisi wa kazi.”

TEKNOLOJIA NA UHALIFU

Kuhusu utayari wa Jeshi la Polisi kukabiliana na matukio ya kihalifu kulingana na teknolojia kupanuka, IGP Sirro alisema katika eneo hilo wanakwenda vizuri ingawa siyo vizuri sana.

Alisema kwa makosa ya kimtandao Jeshi la Polisi linahitaji mafunzo zaidi na ameshazungumza na Mtandao wa Polisi Kimataifa Interpol ili kuwanoa askari wake kimafunzo.

“Tunapata mafunzo sana kwenye suala la uhalifu wa kimtandao, uhalifu huu unahitaji mafunzo mengi kama ulivyo ugaidi unaotokea nchi za jirani, nimeomba waje kutusaidia, pia wameahidi tuvipate baadhi ya vifaa,” alisema.

Alisema makosa hayo yanahitaji nguvu zaidi kwa sababu ni makosa ambayo Tanzania haijawahi kuwa nayo siku za nyuma.

“Tuna upungufu kwenye matukio makubwa lakini siyo kwamba tunashindwa kuyashughulikia, tunahitaji mafunzo zaidi kwa ajili ya kuongeza ujuzi na uelewa zaidi,” alisema na kuongeza:

“Hakuna tukio ambalo litatokea tukashindwa kulishughulikia ndiyo maana utaona mwaka jana kuanzia mwezi Novemba hadi Desemba majambazi hawakuthubutu, sikusikia bunduki mjini wala wapi, lazima Watanzania wajiulize haya hayakutokea siyo kwa sababu tumekwenda kanisani kuomba tu, kuna kazi zinafanyika.”

IGP lisema Januari kila mwaka jijini Dar es Salaam huwa kuna shida ya matukio ya uhalifu, lakini safari hii hayajatokea hadi amejiuliza bunduki zimekimbilia wapi.

Afunguka kuhusu mauaji ya Njombe

Kuhusu matukio ya Njombe, IGP aliwaomba Watanzania waendelee kuchapa kazi kwa sababu matukio hayo hutokea mara moja moja na hutokana na jamii ya eneo husika kuwa na tatizo.

“Jamii ikishasema hiki hatutaki kwa mfano, maeneo wanayovuta bangi, hayatakuwapo jamii ikikaa kimya halafu mtu akavuta bangi akawa kichaa ndipo mtutaarifu tutamchukua na kumpeleka hospitali, kwa nini msitupe taarifa mapema,” alisema.

“Kwa mfano mauaji ya Njombe kama tungepewa taarifa vizuri kwa mfano lile tukio la kwanza ugomvi wa familia baba kamuudhi kijana wake, akaamua kuchukua wadogo zake watatu akaenda kuwachinja, yule baba alitakiwa ajue mbona hapa pana ugomvi nafanyaje kuumaliza kifamilia,” alisema.

Habari Kubwa