IGP: Mikutano ya ndani vyama vya siasa haijapigwa marufuku

17Jul 2019
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam
Nipashe
IGP: Mikutano ya ndani vyama vya siasa haijapigwa marufuku

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, (IGP) Simon Sirro, amesema mikutano ya ndani ya vyama vya siasa haijapigwa marufuku kama inavyozungumzwa.

Akizungumza na askari kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Tabora jana, IGP Sirro alisema mikutano hiyo inaweza kusitishwa tu pale itakapoonekana kwamba kuna viashiria vya uvunjifu wa amani.

"Mikutano ya ndani halijapigwa marufuku popote ila kama kuna taarifa za tishio la usalama kwenye mkutano huo tunaweza kuzuia kwa faida ya Watanzania," alisema.

IGP Sirro alisema mikutano hiyo inaruhusiwa kunapokuwa na mazingira ya amani na kwamba wahusika wanachotakiwa kuzingatia ni kufuata sheria na taratibu zilizowekwa kila wakati.

"Tunapokuwa tumezuia mikutano ya ndani watu wazingatie sheria na watii kwa sababu askari wanakuwa na taarifa zinazoweza kusababisha vurugu sasa tunawataka wahusika watii amri za polisi," alisema IGP Sirro.

Alisema imekuwa kawaida kwa baadhi ya wanachama wa vyama vya upinzani kupiga kelele na kupinga hatua ya askari kuzuia mikutano ya ndani hali inayosababisha amani kutoweka kwenye eneo husika.

"Usipotii tunakushughulikia kwasababu hapo unakuwa umesababisha vurugu kwa kujua au kwa kutokujua, lakini sisi tunakushughulikia kama mhalifu tu kwasababu umefanya fujo na hapo usililaumu jeshi," alisema Sirro.

Kuhusu mikutano ya hadhara, IGP Sirro alisema Rais John Magufuli, alisharuhusu wabunge wafanye mikutano kwenye majimbo yao kwa sharti la kutoa taarifa kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya.

Juzi Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu, lilisambaratisha kwa mabomu ya machozi semina ya kuwajengea uwezo wanawake wa Baraza la Wanawake Chadema (BAWACHA).

Julai 14, Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee, alikamatwa na polisi mkoani Kagera wakati wa ziara yake ya kukutana na wanachama wa Bawacha Mkoa wa Kagera.

Hata hivyo, juzi Mdee aliachiwa kwa kudhaminiwa na watu wawili na ametakiwa kuripoti polisi mkoani humo baada ya mwezi mmoja.