IGP Sirro asisitiza usajili wa kampuni binafsi kwenye mfumo

06Jul 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
IGP Sirro asisitiza usajili wa kampuni binafsi kwenye mfumo

INSPEKTA Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro, ameziagiza kampuni binafsi za ulinzi na wafanyakazi wa kampuni hizo kuhakikisha wamesajiliwa kwenye Mfumo wa Kusimamia Sekta ya Ulinzi Binafsi (PSGP) hadi kufikia Desemba 31, 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufanya kikao na wamiliki na wakurugenzi wa kampuni binafsi za ulinzi nchini wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, IGP Sirro alisema mfumo huo wa kusajili kampuni na wafanyakazi wake kwenye kanzi data maalum ndiyo njia ya kipekee ya kudhibiti changamoto katika sekta hiyo hususan askari wasio waaminifu.

Alisema mfumo huo ni mzuri na utaboresha sekta hiyo, lakini alisisitiza kuwa elimu zaidi inahitajika kwa wadau.

“Mfumo ni mzuri, lakini kitu kikubwa ni suala la elimu. Watu wakielimishwa nadhani wanaelewa, wakurugenzi wangu (wa kampuni binafsi za ulinzi) wana elimu kubwa na wamekwenda shule wakipata elimu ya kutosha wataukubali mfumo,” alisema Sirro.

“Kwa sababu askari leo anafanya uhalifu kwenye kampuni hii na anakwenda kwenye kampuni nyingine kufanya kazi, sasa bila kuwa na mfumo huu huwezi kumtambua huyu askari kwamba ni mbabaishaji,” aliongeza.

Aliwaonya baadhi ya walinzi ambao huingia kwenye sekta hiyo wakiwa na lengo la kupeleleza njia zinazoweza kuwasaidia kufanya uhalifu, na kwamba kupitia mfumo wa PSGP watadhibitiwa.

“Kuna baadhi ya askari hawa wa ulinzi binafsi anaingia kufanya kazi kwa lengo la wizi tu, anapelekwa kule anakuwa chambo kujua kinachofanyika ni kitu gani, lakini kwa kutumia mfumo wa PSGP ndiyo njia ya kipekee ya kuweza kudhibiti hili,” alifafanua.

IGP aliwaagiza wadau wa sekta ya ulinzi binafsi kukutana tena, kuhakikisha wanatatua dosari zilizopo ili wote kwa pamoja wakubaliane na mfumo huo.

Jeshi la Polisi liliagiza kampuni zote binafsi za ulinzi pamoja na wafanyakazi wa kampuni hizo kuhakikisha wamesajiliwa kwenye PSGP kabla ya mwaka 2021, kwani baada ya Desemba 2020 ambao hawatakuwa wamesajiliwa kwenye mfumo huo hawataruhusiwa kufanya kazi kwenye sekta hiyo.

PSGP imeasisiwa na vyama vinavyosimamia sekta ya ulinzi binafsi, na kutekelezwa na Kampuni ya Datavision International chini ya usimamizi wa Jeshi la Polisi.

Mfumo huo unatumia teknolojia kuwasajili kwenye kanzi data kampuni pamoja na wafanyakazi wa kampuni binafsi za ulinzi, na unasaidia upatikanaji wa taarifa za wadau hao kwa haraka ikiwa ni pamoja na kufahamu historia ya mlinzi husika, afya, tabia na mambo mengine.

Zaidi ya kampuni 174 na wafanyakazi 14,000 wamesajiliwa kwenye mfumo huo hadi kufikia siku ya kikao hicho na usajili unaendelea katika mikoa yote nchini.

Habari Kubwa