IGP Sirro aula tena polisi kimataifa

19Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
IGP Sirro aula tena polisi kimataifa

SHIRIKISHO la Wakuu wa Polisi Mashariki Mwa Afrika (EAPCCO) wamemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro, kuendelea kuwa mwenyekiti wake kwa kipindi kingine cha mwaka mmoja.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Wakuu wa Polisi Mashariki Mwa Afrika (EAPCCO) ambaye pia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Simon Sirro (Pichani), akifuatilia mkutano mkuu wa 22 wa mwaka uliofanyika kwa njia ya mtandao (video conference). Katika mkutano huo, IGP Sirro ameongezewa mwaka mmoja kuongoza Shirikisho hilo la Wakuu wa Polisi Mashariki Mwa Afrika. PICHA: POLISI

Kutokana na ombi hilo, IGP Sirro amekubali kuendelea kutekeleza jukumu hilo huku akielezea mafanikio yaliyopatikana kwa mwaka mmoja aliokuwa madarakani.

Uamuzi huo ulitolewa jana na nchi 14 wanachama wa shirikisho hilo kupitia mkutano wake mkuu wa 22 wa mwaka uliofanyika kwa njia ya mtandao (video conference).

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi nchini ilisema jana kuwa Sirro amekubali ombi hilo huku akibainisha kuwa shirikisho hilo limepata mafanikio makubwa.

Pia Sirro alikaririwa akisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2020/21 wamejipanga kutekeleza yale ambayo hayakufikiwa na watahakikisha kuwa nchi wanachama zinabadilishana uzoefu na kufanya mafunzo ya pamoja ya mbinu za medani.

Aidha, katika kikao chake na waandishi wa habari jijini Dodoma, IGP Sirro alisema ushirikiano na wakuu wa polisi Mashariki Mwa Afrika umewezesha kudhibiti uhalifu wa kupanga na unaovuka mipaka.

IGP Sirro aliyataja mafanikio mengine kuwa ni udhibiti wa usafirishaji wa nyara za serikali sambamba na kudhibiti biashara haramu ya usafirishaji binadamu na dawa za kulevya.

IGP Sirro anaendelea tena kuongoza shirikisho hilo kwa kipindi kingine cha mwaka mmoja tangu pale alipochaguliwa katika mkutano mkuu wa 21 wa mwaka uliofanyika mwezi Septemba mwaka jana jijini Arusha.

Habari Kubwa