IPP Media yanyakua Tuzo 7 Umahiri wa Uandishi

30Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Tanga
Nipashe
IPP Media yanyakua Tuzo 7 Umahiri wa Uandishi

​​​​​​​WAANDISHI wa habari wa IPP Media, wameng’ara katika tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2019, kwa kuzoa tuzo saba, katika mashindano yaliyoshindanisha waandishi 56 kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Walioshinda tuzo hizo kwa kushika nafasi za kwanza ni Sanula Athanas, Gwamaka Alipipi, Christina Mwakangale, Abdul Kingo na Rahma Suleiman (wote Nipashe), Crispin Gerald (The Guardian) na marehemu Agnes Almasy wa ITV.

Wengine walioshinda nafasi ya pili na ya tatu katika makundi mbalimbali ni Ashton Balaigwa (Nipashe- Morogoro), Marco Maduhu (Nipashe-Shinyanga) pamoja na Muhidini Msamba na James Kandoya wa The Guardian.

Awali, akizungumza katika utoaji wa tuzo hizo jijini hapa juzi, mmoja wa majaji katika shindano hilo, Pili Mtambalike, alisema ipo haja ya kuwaongezea uwezo waandishi wa habari katika kuandika habari za uchunguzi (IJ).

"Juhudi za ziada na wadau zinahitajika ili kuwajengea uwezo waandishi, sababu ndio inajenga sifa na umahiri wa chombo, IJ uandishi wake umepungua kwa kiasi kikubwa, japokuwa kuna changamoto katika 'media' nyingi," alisema Mtambalike.

Alisema katika mchakato wa kuwapata washindi, baadhi ya masuala jopo la majaji lilibaini changamoto ya kiuandishi, na kwamba lengo la tuzo hizo ni kutambua kazi zenye umahiri katika uandishi.

"Baadhi ya habari zilikuwa na vyanzo anuai. Vyanzo ambavyo vilitumika zaidi ni 'officialls' (wasemaji wa serikali) yaani RCs, wakuu wa wilaya, polisi lakini sauti za kijamii hazikupewa kipambele.”

“Kuna umakini mdogo kwa baadhi ya waliowasilisha kazi zao, mfano walioleta CD hazikuwa na kitu yaani 'empty' inaonekana hawakuwa makini. Redio, televisheni na magazeti hazikuwa na 'back ground' (kueleza kilichotokea nyuma) inaonekana habari hizi hakuna uzingatiaji katika hili," alisema Mtambalike.

Kuhusu kazi za runinga, alisema mahojiano ya vipindi mazungumzo yalimpoka muongoza kipindi na kumuachia mgeni aliyealikwa studio kuongea muda mrefu.

Sanula ambaye ni Mhariri wa habari wa Nipashe, alishinda tuzo mbili katika kipengele cha mwandishi bora wa Habari za Utalii na Uhifadhi, Habari za Haki za Binadamu na  Utawala Bora na kushika nafasi ya pili katika Habari za Elimu.

Pia Christina Mwakangale alishinda tuzo ya kipengele cha Habari za Jinsia na Afya ya Uzazi huku Gwamaka Alipipi akishinda, Habari za Athari za Kemikali kwa Afya ya Binadamu na Mazingira.

Rahma Suleiman, alishinda mshindi wa kwanza tuzo ya mwandishi bora, Habari za Jinsia na kushika nafasi ya tatu kwenye kipengele cha Habari za Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Wengine ni Crispin Gerald, aliyeshinda tuzo ya Habari za Usalama Barabarani huku marehemu Agnes Almasy wa ITV, akishinda tuzo ya Habari za Madhara ya Kemikali kwa Afya na Mazingira kwa upande wa runinga.

Washindi wengine ni James Kandoya wa gazeti la The Guardian, aliyeshika nafasi ya tatu habari za usalama barabarani na Ashton Balaigwa (Nipashe), alishika nafasi ya pili kipengele cha Habari za Utalii na Uhifadhi.

Mchoraji wa Katuni Bora wa mwaka ni Abdul Kingo, aliyeshinda nafasi ya kwanza na ya pili, wakati Muhidini Msamba, akikamata nafasi ya tatu.

Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, alisema tuzo hizo zimechelewa kutolewa mwaka huu kutokana na changamoto ya kifedha na janga la corona.

Alisema tuzo hizo ni za 11 tangu zilipoanzishwa mwaka 2009, na kwa mara ya kwanza zimetolewa nje ya Jiji la Dar es Salaam na kusisitiza kuwa utaratibu huo utaendelea miaka inayofuata.

"Mwaka huu tumetoa tuzo jijini Tanga, tuna imani miaka mingine zitafanyika kwenye mikoa mingine, na si tu Dar es Salaam kama ilivyozoeleka," alisema Mukajanga.

Habari Kubwa