IPP wang'ara tuzo umahiri

14May 2018
Elizaberth Zaya
DAR ES SALAAM
Nipashe
IPP wang'ara tuzo umahiri

WAANDISHI wa habari wa IPP Media waling'ara juzi baada ya kushinda mara tano katika vipengele 16 vya Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari (EJAT) kwa mwaka jana.

Abdul Kingo (Mchora Katuni Bora) na Salome Kitomari aliyeshinda kipengele cha Utalii na Uhifadhi.

Kati ya waandishi wa habari 11 walioteuliwa kuingia kushindania tuzo hizo jijini Dar es Salaam, watano walishika nafasi za kwanza katika vipengele mbalimbali, huku sita wakishika nafasi za pili.

Walioshika nafasi za kwanza ni Salome Kitomari aliyeshinda kipengele cha Utalii na Uhifadhi, Gerald Kitabu (Kilimo na Kilimo Biashara), Abdul Kingo (Mchora Katuni Bora), wote wa magazeti ya Nipashe na la Kiingereza la The Guardian.

Washindi wengine ni Godfrey Monyo (Uhifadhi na Utalii kwa upande wa televisheni) na Peter Rogers (Mpiga Picha Bora wa Televisheni), wote kutoka kituo cha ITV Super Brand.

Rahma Suleiman (Uchumi na Biashara), Abdul Mitumba (Kilimo na Kilimo Biashara), na Maloda Mandago (Habari za Takwimu) kutoka gazeti la Nipashe walishika nafasi za pili katika vipengele hivyo.

David Chikoko wa The Guardian alishika nafasi ya pili katika kipengele cha Mchora Katuni Bora akifuatiwa na Muhidini Msamba wa Nipashe.

Kipengele cha Mchora Katuni Bora kilishindaniwa na wachoraji kutoka IPP Media pekee nchi nzima.

Aidha, Sebastian Kolowa alishika nafasi ya pili katika Utalii na Uhifadhi, upande wa televisheni.

Kitomari na Kitabu walifanikiwa pia kuingia katika kinyang'anyiro cha Mshindi wa Jumla wa tuzo za EJAT ambapo mshindi alikuwa Vivian Pyuza kutoka Redio CG FM ya Tabora.

Akizungumza wakati wa kutangaza washindi hao, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya EJAT, Kajubi Mkajanga, alisema jumla ya kazi 545 zilizochapishwa mwaka jana ziliwasilishwa katika makundi 16 yaliyokuwa yakishindanishwa.

Alisema kati ya kazi hizo zilizowasilishwa, za wanaume zilikuwa 339 sawa na asilimia 62.2 na za wanawake zilikuwa 206 sawa na asilimia 37.8.

Alitaja vipengele vilivyokuwa vikishindaniwa  katika tuzo hizo kuwa ni uandishi wa habari za biashara uchumi na fedha, michezo na utamaduni, habari za afya, kilimo na biashara za kilimo, elimu, utalii na uhifadhi pamoja na habari za uchunguzi.

Nyingine ni habari za takwimu, haki za binadamu na utawala bora, mpiga picha bora wa magazeti, mpiga picha bora runinga, mchora katuni bora, jinsia na vijana, habari za wazee, kodi na mapato na kundi la wazi.

Mwenyekiti wa jopo la majaji, Ndimara Tegambwage, alisema yapo maeneo matatu ambayo bado yanapwaya ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ikiwamo kipengele cha kodi na ukusanyaji wa mapato, kilimo na kilimo biashara na uandishi wa data.

Profesa Issa Shivji alisema bado waandishi wa habari wanafanya kazi katika mazingira magumu na kwamba kunahitajika juhudi za dhati za kuweka mazingira rafiki hasa ya kisheria ya kufanyia kazi zao.

“Tunafahamu kwamba sheria kandamizi ziko katika nchi nyingi duniani, lakini Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo ambazo waandishi wa habari wanafanya kazi katika mazingira magumu sana hasa ya kisheria ambazo pia hata ukizisoma zinakutisha,” alisema Profesa Shivji.