Iringa yakusanya shilingi Bilioni 52.888

16May 2019
George Tarimo
IRINGA
Nipashe
Iringa yakusanya shilingi Bilioni 52.888

MAMLAKA ya Mapato nchini (TRA) Mkoa wa Iringa  imesema umefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 52.888 sawa na asilimia 87 ambapo kwa mwaka wa fedha wa 2017/18 mkoa huo uliweka lengo la kukusanya kiasi cha shilingi Bilioni 60.734.

Kauli hiyo imetolewa na Ofisa Mwandamizi huduma na elimu kwa mlipa kodi Mkoa wa Iringa Barnabas Masika kwenye maadhimisho ya siku ya huduma ya elimu kwa mlipa kodi iliyofanyika Mjini Iringa.

Ofisa huyo amesema kuwa mwaka 2018/19 mkoa huo una lengo la kukusanya kiasi cha Bilioni 60.393 ambapo hadi sasa kuanzia mwezi wa saba mwaka jana hadi mwezi wa nne wamefanikiwa kukusanya kiasi cha Bilioni 48.907 ambayo ni sawa na asilimia 99.8 ukilinganisha na kipindi kama hicho cha mwaka jana.

Masika alisema hadi sasa kuna ongezeko la Bilioni sita ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 16.6.

Alisema kuwa mkoa una mikakati mbalimbali ili kuhakikisha wanafikia malengo ya mkoa  ikiwamo kuboresha huduma zao kwa kutoa elimu kwa walipa kodi na wananchi kwa ujumla,kuendeleza ushirikiano kwa wadau mbalimbali,kufuatiliya matumizi ya mashine za kodi za kieletroniki (EFD’s) na kuongeza wigo wa kodi katika mkoa wa Iringa na kutafuta vyanzo mbalimbali vya mapato.

Naye naibu mkurugenzi wa rasilimali watu na utawala bora Alice Lukindo amewahimiza wafanyabiashara mjini Iringa kutoa risiti kwa wateja wao pindi wanapouza bidhaa zao.

“Ndugu zangu kuna baadhi ya wafanyabiashara hawatoi risiti kwa wateja wao hilo ni kosa la jinai na sisi kama Tra tukimkamata mfanyabiashara kama huyo tutamshughulikia kama sheria inavyotaka na ninyi wanunuzi pendeni kuchukuwa risiti kwa sababu ni haki yenu.”alisema Lukindo

Nao baadhi ya wafanyabiashara wa Mjini Iringa wakiwamo Sophia Nziku na Jumanne Rashid wameilalamikia TRA kwa kuwawekea utitiri wa kodi pamoja na mashine za kieletroniki kuuzwa kwa bei kubwa jambo ambalo wengi wao wanashindwa kumudu gharama.

Rashid alisema kuwa wafanyabiashara wengi sio kwamba hawapendi kulipa kodi ila kinachowakwamisha ni kukosekana kwa elimu juu ya kulipa kodi.

Habari Kubwa