Jafo aagiza mweka hazina, ofisa utumishi waondolewe kazini

07Dec 2019
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Jafo aagiza mweka hazina, ofisa utumishi waondolewe kazini

Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za mitaa Selemani Jafo amemuagiza katibu wake mkuu kuwaondoa kazini Ofisa utumishi wa manispaa ya Shinyanga Magedi Magezi pamoja na Mwekahazina Paschal Makoye, wafanyiwe mabadiliko na kuwapeleka sehemu nyingine wakafanye kazi.

Amesema hajalizishwa na utendaji kazi wa watumishi katika manispaa ya Shinyanga, ambapo kuna makundi makundi na hakuna umoja wa kufanya kazi, ikiwa kila mtumishi ana sauti kama utawala wa kambale, na kubainisha atafanya mabadiliko ya watumishi kwenye idara mbalimbali ambao hawafanyi kazi vizuri..

Jafo amebainisha hayo leo wakati akipokea taarifa ya mkoa wa Shinyanga, kwa mkuu wa mkoa huo Zainab Telack, alipowasili mkoani humo kwa ajili ya kufanya ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya halmashauri ya wilaya ya Shinyanga.

Alisema kutokana na kuwepo na utendaji kazi mbovu katika manispaa ya Shinyanga, ana muagiza katibu wake mkuu, afanye mabadiliko ya kuwondoa kazini Ofisa utumishi pamoja na Mwekahazina, na kupelekwa sehemu zingine wakafanye kazi , ili kuondoa makundi na kushindwa kufanya kazi vizuri ya Serikali.

“Mkuu wa mkoa kwanza na kupongeza kwa kazi nzuri ambayo unaifanya, lakini kwenye manispaa yako ya Shinyanga silizishwi na utendaji kazi wa watumishi kuna tabia ya makundi makundi, hivyo na muagiza katibu mkuu wagu afanye mabadiliko ya kumuondoa Ofisa utumishi pamoja na Mwekahazina,”amesema Jafo.

“Hatuwezi kuwa na watumishi kila mtu ni Kambale, tunafanya madiliko haya ili kazi ifanyike tuwe na Team work na siyo makundi, pia tutaendelea kufanya mabadiliko hayo kwenye halmashauri zote nchini. na jukumu langu mimi ni kumsaidia Rais John Magufuli kuzinyoosha halmashauri,”ameongeza.

Katika hatua nyingine amepongeza ujenzi wa hospitali ya wilaya ya halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kwa hutua nzuri ilipofikia, na kubainisha majengo yake yamejengwa kwa kiwango kinachotakiwa, huku akisema Rais John Magufuli wamewaongeza fedha nyingine Shilingi Milioni 500 ili kuongeza majengo mengine.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Shinyanga Zainab Telack, akisoma taarifa ya mkoa huo, amesema Serikali ilitoa kiasi cha Shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kujengwa hospitali mbili za wilaya mkoani humo, ikiwamo hiyo ya halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambayo imetumia kiasi cha Bilioni 1.5 na imekamilika kwa asilimia 90.

Habari Kubwa