Jafo aagiza walimu wapya walipwe

23Jan 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Jafo aagiza walimu wapya walipwe

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo, ametoa wiki moja kwa halmashauri nchini ambazo hazijawapa fedha za kujikimu walimu wapya, kuhakikisha wanawalipa ndani ya muda huo.

Jafo alitoa agizo hilo jana jijini hapa alipozungumzia uboreshaji wa shule za ufundi nchini.

Alisema mwishoni mwa mwaka jana, serikali iliajiri walimu 13,000 ambao walipangwa kwenye shule mbalimbali nchini na halmashauri ziliagizwa kulipa fedha za kujikimu kwa wakati pindi watakaporipoti kwenye shule walizopangwa.

Hata hivyo, alisema kuna halmashauri hadi sasa bado hazijawapa fedha hizo na kutoa siku saba kuwalipa walimu hao.

"Sitaki kuona wanafanya kazi wakiwa na msongo wa mawazo, ninatoa wiki moja kwa halmashauri ambazo hazijalipa fedha hizo," aliagiza.

Akizungumza kuhusu uboreshaji wa shule za ufundi, Waziri Jafo aliwaagiza wakuu wa mikoa tisa yenye shule za ufundi za sekondari za serikali, kuhakikisha wanakuwa walezi wa shule hizo ili zitoe vijana wenye umahiri wa kutosha na wabobezi kwenye fani mbalimbali.

Alisema serikali imetumia Sh. bilioni 16.4 kukarabati miundombinu ya shule hizo.

Alifafanua kati ya fedha hizo, Shule ya Bwiru ilipewa Sh. milioni 825, Chato Sh. bilioni 3.9, Ifunda Sh. bilioni 3.6, Iyunga Sh. bilioni 1.01, Moshi Sh. bilioni 2.1, Mtwara Sh. bilioni 1.3, Musoma Sh. bilioni 1.2, Mwadui Sh. milioni 226 na Tanga Sh. bilioni 2.1.

Waziri Jafo alisema wakuu hao wa mikoa wenye shule hizo wanapaswa kuzitembelea na kuzungumza na walimu ikiwa ni pamoja na waajiriwa wapya ili kueleza kwa mapana mikakati ya serikali ya kuinua ubora wa shule hizo.

Alisema Sh. milioni 30 zimetengwa kwa kila shule kwa ajili ya ununuzi wa mitambo na vifaa vya kufundishia na kujifunzia katika shule zote hizo za ufundi za sekondari za serikali.

"Baada ya Rais John Magufuli kutangaza na kutoa dira ya kuelekea uchumi wa viwanda mwaka 2016, Ofisi ya Rais TAMISEMI ilichukua hatua mbalimbali, ili kufanya maandalizi ya wataalamu ambao baadaye watatumika katika viwanda vinavyoendelea kujengwa nchini," alisema.

Alisema wataalamu hao watatoka katika shule hizo za sekondari za ufundi ambapo hatua zimechukuliwa ili kuimarisha utoaji wa elimu ya ufundi na kuifanya iendane na mahitaji na ushindani katika ulimwengu wa ajira ili kuongeza pato la mwananchi wa taifa kwa ujumla.

Alisema ili kuhakikisha ufundishaji na ujifunzaji katika shule hizo, Novemba mwaka jana, serikali iliajiri walimu 150 wa masomo ya ufundi wa fani mbalimbali kwa wastani wa walimu 16 kila shule.

Alifafanua kuwa Bwiru (walimu 16), Chato (walimu 18), Ifunda (walimu 16), Iyunga (walimu 17), Moshi (walimu 17), Mtwara (walimu 15), Musoma (walimu 16), Mwadui (walimu 18) na Tanga (walimu 17) na tayari fedha zimetengwa kwa ajili ya kuwajengea uwezo.

Aliongeza kuwa kwa kuwa maboresho yaliyofanyika katika shule hizo ni makubwa huku akitoa wito kwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri wenye shule hizo kuhakikisha miundombinu na vifaa vinatunzwa.

Habari Kubwa