Jafo acharukia mikoa isiyofikia lengo viwanda

21Mar 2019
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Jafo acharukia mikoa isiyofikia lengo viwanda

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, ameijia juu baadhi ya mikoa ambayo imeshindwa kufikia lengo la ujenzi wa viwanda 100 kila mkoa kwa mwaka na kuagiza ifikapo Juni, mwaka huu wawe wamefikia lengo hilo.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, picha mtandao

Jafo aliyasema hayo juzi jijini hapo wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa viwanda 100 kwa kila mkoa kwa kipindi kinachoishia Desemba 2018.

Waziri Jafo alionyesha kutofurahishwa na hali hiyo, huku akisema hataitaja mikoa hiyo hadi mwezi Juni kama watakuwa bado hawajafikia lengo.

"Sijafurahishwa na mikoa hiyo na inajijua haijafikia malengo ya ujenzi wa viwanda 100 nawapa muda hadi mwezi wa sita mwaka huu, mhakikishe mmefikia malengo mliyowekewa, sitaitaja nimetumia busara za uongozi ingawa kiukweli sijafurahishwa sana, mkishindwa kufikia lengo nitawataja hadharani," alisema Jafo.

Waziri Jafo alisema ujenzi huo ni utekelezaji wa mpango wa pili wa maendeleo wa miaka mitano wa mwaka 2016/2017-2020/2021, unaojikita katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, ambao kwa kuanza kila mkoa ulitakiwa kuanzisha viwanda 100.

Alisema hadi kufikia Desemba 31, 2018, viwanda vilivyokuwa vimejengwa kwa nchi nzima vilikuwa 4,777 sawa na asilimia 183.73 ya lengo la kujenga viwanda 2,600 licha ya baadhi ya mikoa kutofikia lengo.

Alisema viwanda hivyo viligawanywa katika makundi manne ambayo ni viwanda vikubwa 108, viwanda vya kati 236, viwanda vidogo ni 2,422, na viwanda vidogo kabisa 2,010, ambavyo vilikuwa vimetoa ajira kwa wananchi 36,796 kwa nchi nzima.

Aidha, Jafo aliutaja Mkoa wa Dar es Salaam kuwa ndio ulioongoza kwa upande wa mikoa iliyofanikiwa kujenga viwanda vikubwa kwa kujenga viwanda vikubwa 46 kati ya 108 vilivyojengwa nchi nzima.

"Ukifuatiwa na mkoa wa Pwani uliojenga viwanda vinane na nafasi ya tatu ikishikwa na mikoa mitatu ambayo ni Mwanza, Lindi na Simiyu ambayo kila mmoja ulijenga viwanda vikubwa saba," alisema.

Alisema mikoa na serikali za mitaa ina wajibu wa kuwatumia kikamilifu wataalamu hasa maofisa maendeleo ya jamii na maofisa biashara waliopo ili kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda na upatikanaji wa malighafi za kutosha.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa wakuu wa mikoa, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, alimhakikishia waziri Jafo kuwa watatekeleza maagizo hayo kikamilifu.

Habari Kubwa