Jafo akerwa kasi kinyonga ukusanyaji mapato Kigoma

16Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Kigoma
Nipashe
Jafo akerwa kasi kinyonga ukusanyaji mapato Kigoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amesema Manispaa ya Kigoma Ujiji inakabiliwa ugoigoi katika ukusanyaji wa mapato hali inayochangia kuzorota kwa shughuli za maendeleo ilhali ina rasilimali za kutosha.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, picha mtandao

Jafo alisema hayo juzi kwenye uzinduzi wa Mfumo wa Kisasa wa Ukusanyaji Mapato kupitia Taarifa ya Kijiografia (GIS) uliounganishwa na mfumo wa mapato wa LGRCIS chini ya Mradi wa TSCP ili kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha za umma.

Alisema ugonjwa unaoisumbua Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji ni 'unyafunzi' wa ukusanyaji wa mapato kupitia vyanzo vyake mtambuka, kitendo kinachokwamisha kutatua kero na changamoto zilizo ndani ya uwezo wake kupitia mapato ya ndani. 

Alisema atashangazwa na manispaa hiyo endapo itashindwa kuonyesha ufanisi katika ukusanyaji wa mapato kwa weledi bila ujanja ujanja unaofanywa na watu wachache wanaohujumu uchumi ambao wanaathiri maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.
 
"Nina sababu kubwa ya kutaka mabadiliko chanya katika ukusanyaji wa mapato. Huu ni mkoa wa kwanza kwa mgeni rasmi kuzindua mradi wa  kisasa wa kitakwimu, uendelezaji na mkakati wa ukuaji wa miji ambao utakusanya mapato kwa mfumo wa taarifa za kijiografia uliounganishwa na mfumo wa mapato wa LGRCIS ili kudhibiti ugoigoi wenye  mianya ya upotevu wa fedha za umma," alisema.

GIS ni kielelezo cha kubaini taarifa za kila mkazi na shughuli anayoifanya na taarifa zitaunganishwa na mfumo wa ukusanyaji wa mapato ili kubaini taarifa za walipakodi, huku akiwapongeza wataalamu wa mfumo huo wa kitakwimu (fungamano).

"Sasa msiichezee mifumo takwimu hii kwa maslahi binafsi. Fanyeni  kama mfumo unavyotaka na tuwe waadilifu katika matumizi ya mfumo wa GIS kwa tija hata mataifa na halmashauri ziige taratibu za kitakwimu.

“Ajenda kubwa ya Rais John Magufuli na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kukusanya mapato yatakayotatua kero na changamoto za wananchi. Wakurugenzi wajibikeni msione haya kuuliza jambo kwa maslahi ya umma," alisema.

Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Mhandisi Mussa Natty, alisema wakusanyaji wa mapato walio wengi ni wadanganyifu wa makusanyo ambayo hayana taarifa ya takwimu za walipa kodi.

Alisema matumizi ya GIS  na LGRCIS yataweka takwimu za kisasa kwa kuwa yanabaini kila mlipa kodi na shughuli ya mkazi, taarifa zote za uzalishaji mali na watumishi wakifuata weledi wataongeza mapato maradufu na halmashauri itaweka historia ya mafanikio kwa maslahi ya umma.

Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Hussein Ruhava, akiri halmashauri hiyo inakabiliwa na changamoto kubwa ya kufanya vibaya katika ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa zaidi ya miaka mitano. 

Alisema mpango huo utatatua changamoto mtambuka na wataitumia fursa ya elimu elekezi waliyopewa na wataalamu wa Tehama kutoka Tamisemi kwa kuwajengea uwezo wa mafunzo juu ya ukusanyaji wa mapato kwa matumizi ya GIS ili wananchi waifurahie serikali.
0000

Maandalizi Stierglers’ Gorge asilimia 40
 
Na Mwandishi Wetu, RUFIJI
 
KAZI mbalimbali za maandalizi ya ujenzi wa mradi wa umeme wa megawati 1,115 katika Mto Rufiji zinazofanywa kwa ubia na Arab Contractors na Elsewedy Electric,  zimefikia zaidi ya asilimia 4O.
 
Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, alisema hayo jana alipokuwa akitoa taarifa ya mradi huo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambao walitembelea eneo la mradi, Rufiji mkoani Pwani.
 
Kamati hiyo ya Bunge pia ilikagua miundombinu wezeshi iliyotekelezwa na serikali ikiwamo barabara, umeme, nyumba za wafanyakazi na sehemu maalumu ya kushushia mizigo Stesheni ya Tazara katika kituo cha Fuga.
 
Dk. Kalemani alisema mkandarasi huyo alianza kazi za maandalizi baada ya kukabidhiwa eneo hilo la mradi Februari, mwaka huu.
 
Alizitaja baadhi ya kazi ambazo mkandarasi  anaendelea kutekeleza kwa sasa kuwa ni ujenzi wa kambi ya muda ya wafanyakazi, uletaji wa vifaa na mitambo itakayotumika wakati wa ujenzi na kazi za kuchukua sampuli za udongo na maji kwa ajili ya utafiti.
 
Aliongeza kuwa baada ya kukamilisha kazi hizo za maandalizi, mkandarasi huyo anatakiwa kumaliza kazi ya ujenzi ndani ya miezi 36.
 
Waziri Kalemani alisema pamoja na kuridhishwa na hatua hiyo ya maandalizi, bado serikali kupitia Wizara ya Nishati itaendelea kumsimamia mkandarasi ili amalize kazi ndani ya muda uliopangwa.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula, baada ya kukagua miundombinu iliyotekelezwa na serikali pamoja na kazi za maandalizi zinazofanywa na mkandarasi, aliipongeza serikali kwa kuamua kuutekeleza mradi huo na kuusimamia kikamilifu.
 
Alisema kamati pia inafuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kukamilika kwa wakati kutokana na umuhimu wake nchini. Pia alitoa wito kwa wizara kutorudi nyuma katika usimamizi wa mradi.
 
Sambamba na hilo, aliwataka wafanyabiashara nchini kuchangamkia fursa zinazopatikana katika mradi kwa kuwa serikali itatumia takribani Sh. trilioni 6.5 kutekeleza mradi huo, hivyo ni muhimu Watanzania wafaidike na fedha hizo.

Habari Kubwa