Waziri Jafo ameyasema hayo Jijini Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Chama cha Msalaba Mwekundu (REDCROSS) Duniani yaliyokwenda sambamba na miaka 60 ya Tanzania Red Cross tangu kuanzishwa mwaka 1962 ambayo yameambatana na zoezi la upandaji wa miti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Waziri Jafo amesema ni muhimu kwa kila Mtanzania kuendelea kulinda amani ya Tanzania kwani kuna baadhi ya mataifa hayawezi kufanya sherehe zozote za maandamano kutokana na machafuko.
"Moyo wa kujitolea katika kusaidia jamii pindi yanapotokea majanga pamoja na zoezi la ushiriki wa upandaji miti ni muhimu ," alisema Jaffo
Pia aliipongeza Red Cross kwa moyo wa kujitolea kwa kuisaidia jamii inapokumbwa na majanga pamoja na kuwapongeza kwa zoezi la upandaji miti na kueleza kuwa kitendo hicho ni cha kizalendo.
Akizungumzia Sensa ya watu na makazi ambayo inatarajiwa kufanyika Agosti 23,2022 ,Waziri Jafo amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi ili serikali iweze kuweka bajeti sahihi kwa ajili ya maendeleo. Naye Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) amesema shirika hilo limekuwa na mashirikiano na serikali ya Tanzania kwa kuungana na makundi muhimu ya kuhudumia jamii ikiwemo Chama cha Msalaba Mwekundu huku mwakilishi wa shirika kuhudumia wakimbizi duniani (UNHCR) akisema Serikali ya Tanzania imekuwa na mchango mkubwa hususan utoaji wa huduma katika kambi za wakimbizi za Kigoma.
Dk. Asha Mohammed, Mwakilishi Redcross Kenya, akizungumza kuhusu kazi zinazofanywa na RedCross alisema kuwa shirika hilo limekuwa kikifanya kazi za kijamii kwa kujitolea pale panapotokea majanga.
Kwa niaba ya Mbunge wa Momba Condester Sichalwe, amekipongeza chama cha Msalaba Mwekundu kwa kuendelea kutoa huduma kwa jamii huku akitoa wito cha chama hicho kufika zaidi vijijini ili wananchi wajue majukumu muhimu yanayotolewa na chama hicho.
Mwakilishi kutoka EXIM Bank ambao ndio wadhamini wakubwa wa maadhimisho hayo alisema benki hiyo tangu ianzishwe miaka mitano iliyopita wamekuwa bega kwa bega katika ushiriki wa huduma za jamii.
Tanzania redcross ilianza mwaka 1948 baada ya vita kuu ya pili vya dunia.