Jafo ataka agenda ya elimu kupitiwa

21Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Jafo ataka agenda ya elimu kupitiwa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amesema Tanzania haiwezi kufikia nchi yenye kipato cha kati bila kupitia agenda ya elimu.

Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo.

Kauli hiyo ameitoa leo Agosti 21, 2019 wakati akizungumza na Maafisa elimu wa mikoa na wilaya mkoani Dodoma.

Amesema kuwa Serikali imekusudia kuleta mapunduzi makubwa sana na hasa katika dira ya Taifa ya mwaka 2020/25 inayoelekeza ifikapo mwaka 2025 tuwe katika nchi yenye kipato cha kati.

"Na hili mnafahamu hatuwezi kuwa nchi yenye kipato cha kati bila kupitia katika agenda ya elimu lakini mpango wetu wa muda mrefu  2011-2012 mpaka 2024-2025 inatuelekeza jinsi gani tujiwekeze katika elimu,’’amesema Jafo

Ameongeza kuwa baada ya ugatuaji wa madaraka hasa katika upande wa elimu ambapo zamani hapakuwa na msimamizi wa elimu maalum na elimu ya watu wazima leo hii imeonekana wazi suala la elimu ya watu wazima sasa kuweza kuwabainisha.

Hata hivyo Jafo amewataka maafisa elimu watakapokutana katika kikao cha kazi wafunguke na kujadili na kubainisha mipango ya nini kifanyike kwa serikali ya awamu ya tano kuyasaidia makundi hayo.

"Tutakapokutana katika kikao cha kazi tutajadili mambo mengi hasa jinsi gani elimu ya watu wazima, elimu jumuishi kwa ujumla wake pamoja na elimu ya mahitaji maalum na hasa nyie ndio watalam mnasimamia hilo nawaomba mfunguke na mbainishe changamoto na nini kifanyike katika serikali ya awamu ya tano kuwasaidia makundi hayo," amesema Jafo 

Amesema kuwa baada ya Rais Magufuli kuelekeza rasmi kuwa makao makuu ya nchi yawe Dodoma imekuwa ni faraja kwa maafisa kukutana mkoani hapo kubadilishana mawazo ili mwisho wa siku kwenda kufanya kazi ambayo ana imani italeta matunda makubwa kwa taifa.

Imeandikwa na Juster Prudence, TUDARCo

Habari Kubwa