Jafo awaonya wakuu wa mikoa

16May 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Jafo awaonya wakuu wa mikoa

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amewataka wakuu wa mikoa kutumia uongozi wao vizuri ili kujiepusha kusababisha madhara kwa kiongozi mkubwa wa nchi.

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo.

Jafo alitoa kauli hiyo juzi alipokuwa akizungumza na wakuu wa mikoa katika kikao cha tathmini ya utoaji wa vitambulisho kwa wajasiriamali nchini.

 

Alisema huwa inampa tabu kiongozi anapowadhalilisha watumishi wa umma kwa kiwango kikubwa.

 

“Naomba muende kulifanyia kazi, sisi sote ni viongozi hakuna mkamilifu hata Mungu anatufahamu, nendeni mkabadilike ili kupata hamasa kwa watumishi na mabadiliko makubwa,” alisema.

 

Aliwataka wawafanye watumishi waliochini yao kuwa na hamu ya kufanya kazi hata saa za ziada.

 

“Inawezekana wakati mwingine mtumishi wa chini anafanya kazi hadi unamuonea huruma, anafanya vile kwasababu ana nguvu ya kutosha anahamasa moyoni ya kufanya kazi, mwingine anaweza kufanya kazi kwa kuogopa na kulazimishwa,”alisema.

 

Waziri huyo alisema si vyema kiongozi kushindwa kutengeneza hamasa kwa watu walio chini yake kwa kuwa watakuwa na watumishi wanaowaongoza wenye hasira na serikali yao.

 

“Licha ya kufanya investment (uwekezaji) kubwa ya miradi yetu huku wananchi inawezekana wapo ‘happy’ (wanafuraha), lakini safu hii ambayo tunawaelekeza wawahudumie wananchi wanawezekana wakawa hawana hamasa ya utendaji kazi,”alisema.

 

Aliwataka kubadilisha utendaji wao wa kazi na kukuza hamasa kwa watumishi.

 

“Naamini tukifanya hivi tutakuwa na jeshi kubwa lenye hamasa ya watu, wale wanaofanya mambo ya ovyo tusiwafumbie macho,”alisema.

Habari Kubwa