Jafo awashukia maofisa utumishi

11Jan 2020
Julieth Mkireri
Kibaha
Nipashe
Jafo awashukia maofisa utumishi

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, amekemea tabia ya baadhi ya maofisa utumishi kuchelewesha taarifa za baadhi ya watumishi pindi wanapopanda madaraja.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, picha mtandao

Jafo aliyasema hayo jana mjini hapa wakati wa maadhimisho ya Miaka 50 ya Shirika la Elimu Kibaha.

Alisema suala la maofisa utumishi kuchelewesha kuandaa miongozo kwa watumishi waliojiendeleza ni shida ambayo iko katika maeneo mbalimbali.

"Miongozo ya watumishi haitengenezwi na wanasiasa, si mkuu wa mkoa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wala Jafo, inatengenezwa na wataalamu wenyewe na wanaolalamika ni wataalamu.

“Maofisa Utumishi mnatuangusha kwa kushindwa kuandaa bajeti kwa watumishi wanaopanda madaraja. Adui wa wataalamu ni wataalamu wenyewe, hata kupanda madaraja ni wataalamu wenyewe,” alisema.

Aidha, Waziri Jafo alimwanguza Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha, Robert Shilingi, kushughulikia changamoto zilizoelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, kuhusu baadhi ya watumishi wa idara ya afya.

Pia alimtaka mkuu wa mkoa kuwasiliana na mamlaka zinazohusika kuhakikisha wanatengeneza ruti maalumu kufika katika Hospitali ya Rufani Tumbi kwa kuwa sasa wagonjwa na wanaokwenda wanalazimika kukodi bajaji, pikipiki na teksi kwa usafiri.

Kuhusu uchakavu wa miundombinu, Waziri Jafo alisema, Serikali imetumia kiasi cha Sh. bilioni 49.9 kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe ikiwamo Kibaha Sekondari.

Awali, Ndikilo alisema watumishi wa Hospitali ya Tumbi baadhi yao wamekuwa wakilalamikiwa kuwa na kauli ambazo si rafiki kwa wagonjwa.

"Tutoeni huduma bora kwa wananchi. Tunalalamikiwa kuwa na lugha chafu kwa wagonjwa. Tunalalamikiwa kama mkoa, tuliokengeuka tujirekebishe," alisisitiza Ndikilo.

Habari Kubwa