Jafo azuia uchenjuaji dhahabu mgodini Mara

18Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Tarime
Nipashe Jumapili
Jafo azuia uchenjuaji dhahabu mgodini Mara

​​​​​​​WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo, amesitisha shughuli za uchenjuaji wa dhahabu katika mtambo wa Double F ulioko Kijiji cha Nyakisya wilayani Tarime kutokana na uchafuzi wa mazingira.

Alitoa uamuzi huo wakati alipokuwa akifuatilia malalamiko ya wananchi kuhusu athari za kiafya na kimazingira zinazotajwa kutokana na kemikali ya Cyanide inayotumika katika shughuli za uchenjuaji wa dhahabu na kutiririka katika chanzo cha maji cha Senye.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa maeneo hayo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyakihenene, Mwita Ngusui, alisema wakazi wengi na vitongoji vya maeneo ya jirani kwa kiasi kikubwa wameathirika na kemikali ya Cyanide

Kutokana na athari hizo, Jafo alisema kikosi kazi kinachoundwa na taasisi za serikali ikiwa ni pamoja na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Mkemia Mkuu na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, kwa pamoja kitachunguza na kutoa taarifa za kitaalamu kuhusu maji hayo ili hatua stahiki zichukuliwe.

Jafo alisema ofisi yake haitamvumilia mwekezaji yeyote anayeharibu mazingira na kuathiri afya za watu.

Katika hatua nyingine, Waziri Jafo alibaini ukikwaji wa Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004 katika mgodi huo wa Double F kwa kuanza shughuli ya uchenjuaji bila kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira.

Alimwelekeza Msimamizi wa mtambo huo, Is-haka Juma, kuwalisiliana na Ofisi za NEMC mapema iwezekanavyo ili ukaguzi wa mazingira ufanyike.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa maeneo hayo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyakihenene, Mwita Ngusui, alisema wakazi wengine wa maeneo hayo na vitongoji vya jirani kwa kiasi kikubwa wameathirika na kemikali hiyo.

Mbunge wa Rorya, Jafari Chege, aliishukuru serikali kwa kusikia kilio cha wananchi wa Rorya kwa kufanya ufuatiliaji wa haraka.

Habari Kubwa