Jaji Mkuu 'alia' uhaba wa majaji

07Feb 2019
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Jaji Mkuu 'alia' uhaba wa majaji
  • *Mmoja anasikiliza kesi 513

JAJI Mkuu, Prof. Ibrahim Juma, amesema mahakama inakabiliwa na uhaba wa majaji, hivyo kuiomba serikali kuitafutia ufumbuzi changamoto hiyo.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwa ndani ya gari maalumu litakalotumika kama Mahakama inayotembea baada ya kuizindua rasmi akiwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Mhe. Job Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Juma,

Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria nchini yaliyohudhuria na viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwamo Rais John Magufuli na Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Prof. Juma alisema majaji wa Mahakama Kuu wana mzigo mkubwa wa kutoa huduma, akibainisha kuwa, kwa sasa  mahakama hiyo inao 73 na kila jaji analazimika kusikiliza kesi 513 kwa mwaka.

Jaji Mkuu pia alisema mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) umesaidia mahakama kupunguza vitendo vya rushwa na umewezesha kufanyika kwa urahisi usimamizi wa mashauri, kuitwa kwenye kesi na kuwezesha kujua kinachofanywa na mahakama.Alisema kupitia mfumo huo, hakuna kesi yoyote inaweza kusajiliwa bila kulipiwa ada na kwamba, maduhuli yameongezeka kutoka Sh. bilioni 1.629 hadi Sh. bilioni 2.164 kati ya Julai na Desemba mwaka jana.Prof. Juma pia alizungumzia mahakama zinazotembea, zinazofadhiliwa na Benki ya Dunia, akieleza kuwa zitaanza kutoa huduma katika mikoa miwili ya Dar es Salaam na Mwanza.Aliyataja maeneo ya Dar es Salaam yatakayofikiwa na mahakama hizo kuwa ni Chanika, Kibamba, Buza na Bunju wakati Mwanza zitatoa huduma Buhongwa, Igoma na Buswelu.

Mratibu wa Mashauri, Eva Nkya, alisema magari hayo yaliyokamilika kama mahakama, kila gari limegharimu Sh. milioni 470.8.

Jaji Mkuu pia aliiomba serikali kumwagiza Mpigachapa Mkuu wa Serikali kuchapisha sheria zote mtandaoni ili wananchi wazisome na ziwasaidie kuelewa wanapofungua kesi mbalimbali zikiwamo za ardhi.

Katika maadhimisho hayo, Rais Magufuli aliagiza wapelelezi wa makosa ya jinai kuacha uzembe na kufanya kazi zao kwa ufanisi ili kuisaidia mahakama katika uotaji haki kwa jamii, akibainisha kuwa, kesi 1,986 zilifutwa kutokana upelelezi kuwa kikwazo.

Rais Magufuli alisema kesi hizo zilifutwa licha ya kuwa na ushahidi wa wazi, lakini kutokana na uzembe wa wapelelezi kushindwa kukamilisha ushahidi, mahakana ilizifutilia mbali."Mwaka 2018 kesi 1,986 zimefutwa kwa sababu ya uzembe wa upelelezi, tufanye kazi tusaidie majaji na mahakimu kutoa haki," alisema.

Alisema anatambua kwamba mahakama inakabiliwa na changamoto mbalimbali na kuahidi serikali kuendelea kuunga mkono juhudi za mhimili huo.

Alisema mahakama inayotembea itaongeza ufanisi wa kazi kwa mahakimu kwa utoaji haki kwa wananchi waliombali na huduma hiyo.

Rais Magufuli pia aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi, bali waweke bidii katika kuzijua sheria za nchi na kuziheshimu.

Vilevile, alisema kuna changamoto ya rushwa, akieleza kuwa wasajili wa mahakama "wana dhambi zao" ikiwamo ya kupanga kesi kwa majaji kwa kuangalia nani mwenye uwezekano wa kupata chochote.

”Mimi nafahamu wasajili, ninyi mna dhambi zenu, mnaangalia kesi hii ina pesa nyingi, unampangia jaji fulani, na hii haina kitu, unampangia jaji fulani, fanyeni kazi kwa weledi," alisema Rais Magufuli.

Aliongeza: “Ninafahamu wajane wanapata shida sana hasa katika masuala ya mirathi, wasikilizeni na kumaliza kesi zao, wanaume waliofiwa na wake zao na wanawake waliofiwa na waume zao, haki zao zisikilizwe jamani, nawaomba sana mkalifanyie kazi.”

Kuhusu changamoto ya uhaba wa majaji, Rais Magufuli alisema kuna mahakimu walioteuliwa chini ya Kifungu cha 73 cha Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA), wana hadhi ya kusikiliza kesi za Mahakama Kuu, hivyo watumike kama mbadala wa majaji ili kuziba mapengo.

Rais Magufuli alisema sekta zote za serikali zinakabiliwa na ubaha wa watumishi, hivyo kuna haja kujiongeza kwa kuangalia mbadala wa upungufu uliopo.

”Naishukuru sana Benki ya Dunia (WB) kwa msaada wa mahakama inayotembea, kwani itamaliza kero ya utoaji haki kwa wakati,” alisema.

Habari Kubwa