Jaji ataja viashiria uchaguzi usio na malalamiko

14Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Jaji ataja viashiria uchaguzi usio na malalamiko

JAJI mstaafu wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, Mbarouk Salim Mbarouk, amesema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kufuatwa, ambazo zinaweka msingi imara wa uchaguzi wenye uwazi na usio na malalamiko au vurugu.

Aliyasema hayo  mjini Chake Chake alipokuwa akifungua mafunzo kwa watendaji wa wasimamizi wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Konde .

Aliwataka wasimamizi hao kufanya kazi kwa ufanisi kwa kuzingatia sheria, kanuni na maelekezo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), huku wakiepuka kufanya kazi kwa mazoea ili kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika katika hali ya amani na utulivu.

Aliwasihi watendaji hao wahakikisha wanawashirikisha wadau wote wa uchaguzi wakiwamo wanasiasa ili kuwe na uchaguzi huru na wa haki.

Mkurugenzi I dara ya Usimamizi wa Uchaguzi NEC, Hamidu Mwangu, aliwataka watendaji hao kuwa makini katika kufuata maelekezo watakayopewa na NEC katika kutekeleza majukumu hayo kwa mujibu wa utaratibu uliopangwa.

Uchaguzi mdogo Jimbo la Konde Wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba ambao unatarajia kufanyika Oktoba 9, mwaka huu, kufuatia kujiuzulu kwa mbunge mteule jimbo hilo, Sheha Mpemba Faki ambae alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi mdogo uliofanyika Julai 18, mwaka huu kufatia jimbo hilo kuwa wazi  baada ya kufariki dunia kwa aliyekuwa mbunge wajimbo hilo, Khatib Said Haji (ACT) Mei 20, mwaka huu.

Faki (CCM), alijiuzulu baada ya uchaguzi huo mdogo kukumbwa na malalamiko kutoka Chama cha ACT-Wazalendo.