Jaji Mihayo awataka wasimamizi wa uchaguzi kujiamini

02Aug 2020
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
Jaji Mihayo awataka wasimamizi wa uchaguzi kujiamini

Waratibu wa uchaguzi mkuu wa mikoa, wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi, maofisa ugavi na maofisa uchaguzi kutoka Mkoa wa Mwanza na Mara wamepewa mafunzo ya siku tatu ya watendaji wa uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji mstaafu Thomas Mihayo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji mstaafu Thomas Mihayo amesema wamewakutanisha ili wabadilishane uzoefu,kujadili namna ya kufanikisha zoezi la uchaguzi mkuu, kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika hatua zote za uchaguzi.

Amesema tume imewaamini na kuwateua kwa sababu wanao uwezo wa kufanya kazi hiyo hivyo wajiamini ,kujitambua na kuzingatia katiba ya nchi,sheria za uchaguzi na kanuni zake , maadili na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na tume katika kutekeleza majukumu yao.

"Taratibu hizo ambazo mtaelekezwa kwenye mafunzo  ndio msingi wa uchaguzi kuwa mzuri na wenye ufanisi hivyo kuzingatia na kutekeleza taratibu hizo kutapunguza kama siyo kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi sambamba na kuzingatia maelekezo ya tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea" ameeleza Jaji mstaafu Mihayo.

Pia amewahimiza kujifunza kwa vitendo mambo muhimu katika mchakato wa uchaguzi ikiwemo ujazaji sahihi wa fomu mbalimbali,ufungaji wa vituturi, kufunga na kufungua masanduku ,mpangilio wa kituo na taratibu za upigaji kura sambamba na kuyajua vyema maeneo yao ya kufanyia kazi ikiwepo hali ya kisiasa na miundombinu ya kufika katika kata na vituo husika.

"Katika utekelezaji wa majukumu yenu, ni muhimu pia mvishirikishe vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi kwa uwazi katika masuala ambayo wanastahili kushirikishwa ili kujenga Umoja kuanzia hatua ya awali hadi siku ya kutangazwa matokeo hii itasaidia kuondoa migogoro,vurugu,uvunjifu wa amani ,kuharibika kwa uchaguzi  na kusababisha hasara kwa serikali na maisha ya watu pia ni muhimu kuhakiki na kubaini mahitaji sahihi ya kila kituo na kutatua changamoto mapema kabla ya siku ya kupiga kura" ameongeza Jaji mstaafu Mihayo.

Naye Mwenyekiti wa mafunzo Kiomoni Kibamba ambaye ni  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza anasema wamejiandaa vyema kupokea mafunzo hayo ,hivyo hawatawaangusha bali wataitendea haki elimu hiyo watakayoipata.

Aidha Mkurugenzi wa Jimbo la Musoma Mjini, Fidelica Myovella akizungumza kwa niaba ya wana mafunzo anaeleza kuwa watatumia muda huo wa siku tatu kusikiliza kwa umakini,uaminifu na utii ili kuhakikisha yote wanayofundwa wanayazingatia lengo likiwa ni kuwafikishia elimu hiyo kikamilifu wenzao katika maeneo ya uchaguzi watakayoenda.

Habari Kubwa