Jaji Mkuu aonya rushwa akiapisha mawakili wapya 

16Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Jaji Mkuu aonya rushwa akiapisha mawakili wapya 

JAJI Mkuu Prof. Ibrahim Hamis Juma, amewaapisha mawakili wapya huku akiwaonya juu ya kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Badala yake, amewataka kuisaidia Mahakama ya Tanzania katika kupambana na rushwa kwa kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya taaluma hiyo.

Akizungumza jana wakati wa sherehe za 57 za kuwakubali na kuwaapisha mawakili wapya zilizofanyika katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam, Jaji Mkuu aliwataka mawakili kutokutumia vifungu vya sheria na kanuni ili kuchelewesha upatikanaji wa haki kwa kuwa suala la upatikanaji wa haki huwategemea wao. 

“Katika karne hii ya 21 ni muhimu kwa mawakili kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa huduma za karne hii huvuka mipaka ya nchi,” alisema.

Prof. Juma pia aliwashauri mawakili kusoma na kuzifahamu sheria za kimataifa ili wawe na upeo mkubwa katika kushughulikia kesi hasa zile zinazohusisha nchi zaidi ya moja. Baadhi ya kesi hizo ni zile zinazohusu mipaka ya nchi, makosa ya kimtandao na zile zinazohusu maliasili.

Aidha, Jaji Mkuu aliyataka baadhi ya makosa ambayo yamekuwa yakifanywa na baadhi ya mawakili na wananchi kuwashitaki kuwa ni kutoa siri za wateja, kughushi nyaraka, kutayarisha mikataba zaidi ya mmoja kwa lengo la kudanganya, wakili kuchukua kesi bila ruhusa ya mteja, kuwaibia wateja kwa kuwatoza fedha nyingi, kuwadanganya, kuchukua kesi yenye maslahi binafsi na uzembe.

Prof. Juma pia aliwashauri mawakili wapya kuhakikisha wanashirikiana na taaluma zingine wanapofanya kazi zao ili kurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa haki kwa wateja wao.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, amewataka mawakili wapya kutosubiri kuajiriwa na serikali na badala yake wajiajiri na kutoa huduma mikoani na si Dar es Salaam peke yake. 

Naye Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Godwin Ngwilimi, aliwataka mawakili nchini kutekeleza wajibu wao kwa kufuata misingi ya haki na kujiepusha na rushwa. 

Mawakili wapya 296 walikubaliwa na kuapishwa jana, hivyo  kufanya idadi ya mawakili nchini kufikia 6,536.  

Habari Kubwa