Jaji Mkuu aonyeshwa kero Majaji

05Mar 2016
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Jaji Mkuu aonyeshwa kero Majaji

Mkazi mmoja wa jijini Dar es Salaam amemtaka Jaji Mkuu, Othman Chande kuangalia uwezekano wa kuwa na mfumo utakaowawezesha upatikanaji wa mapema wa hukumu za majaji na mahakimu ili kuondoa usumbufu kwa wananchi.

Jaji Mkuu, Othman Chande (KUSHOTO).

Akizungumza na Nipashe juzi jijini, Mariam Meghjee aliyedai kuwa na kesi ya ardhi namba 67 ya mwaka 2010, alisema amekuwa akisuburi kupata nakala ya hukumu yake kutoka Mahakama Kuu kwa mwezi mmoja sasa wakati muda wa kukata rufaa ni ndani ya siku 30.

Amesema wananchi wengi wanaofuatilia nakala za hukumu katika Mahakama Kuu wamekuwa wakizungushwa.

Kesi inayomlazimisha kusotea nakala ya hukumu hiyo ilifunguliwa katika Mahakama Kuu na Kampuni ya Alisum Properties Limited dhidi ya Selenda Msangi, alisema, na kwamba ilidumu kwa miaka sita kabla ya kutolewa hukumu yake Februari 5, mwaka huu.

Mariam alisema anashangaa kuona wakili wake akizungushwa kupata hukumu iliyotolewa kwa kusoma maandishi, huku siku 30 za mlalamikaji kukata rufaa zikimalizika.

“Unajua sielewi kinachoendelea kuhusu nakala ya hukumu," alisema Miriam. "Jaji anazunguka nayo kwenye komputa mpakato (laptop) kila siku!"Hiyo siyo haki hata kidogo, Jaji Mkuu atusaidie kuchukua hatua.”

Usumbufu anaopata yeye katika kufuatilia nakala ya hukumu ndiyo unaowakuta watanzania wengine, alisema na hivyo changamoto hiyo inapaswa kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Mariam alisema kutokana na ufinyu wa uelewa wa tafsiri za kisheria, wananchi wengi huamini tatizo hilo linasababishwa na rushwa, kwamba ili apatiwe nakala ya hukumu ni lazima mhusika atoe rushwa.

Naibu Msajili Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Charles Magesa alikiri ucheleweshwaji wa utoaji wa nakala za hukumu, hasa kutokana na wingi wa idadi ya kesi zinazoamriwa na jaji kwa siku.

Alisema zipo baadhi ya kesi zinazotolewa hukumu yenye kurasa zaidi ya 100 hivyo Jaji hulazimika kuwapatia makarani kupiga chapa nakala hizo za hukumu.

“Ni kweli wapo majaji ambao kabla ya kutoa hukumu huchapa nakala hizo, lakini majaji wengine hutegemea wengine (makarani) kufanyakazi kazi hiyo,” alisema Magesa.

Iwapo mwananchi atakuwa anahitaji nakala ya hukumu, alisema Magesa, anapaswa kuandika barua kwa Msajili au kumtumia wakili wake kufuatilia mahakamani.

Habari Kubwa