Jaji Mkuu ataka dhamana watuhumiwa kesi mauaji

20Jul 2019
Beatrice Moses
Dar es Salaam
Nipashe
Jaji Mkuu ataka dhamana watuhumiwa kesi mauaji

JAJI Mkuu wa Tanzania,Ibrahimu Juma, amesema mahakama inapendekeza kesi zote zikiwamo za mauaji ziwe na dhamana kwa watuhumiwa ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kukabiliana na msongamano wa wafungwa na mahabusi magerezani.

JAJI Mkuu wa Tanzania,Ibrahimu Juma.

Kiongozi huyo wa mahakama aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akiwaapisha mawakili 720. Alisema suala hilo linawenzaka kama ilivyo katika nchi ya Kenya ambayo dhamana inatoka kwenye kesi zote zikiwamo za mauaji.

“Sisi kama mahakama tuna mapendekezo tuwe kama Kenya, makosa yote yapewe dhamana. Mahakama iachiwe haki ya kusimamia dhamana, yaani sheria isifunge dhamana, hatutakuwa na hilo tatizo (msongamano wa wafungwa na mahabusi). Kenya tumeona mahakama inatoa dhamana kwenye kesi za mauaji, hilo linawezekana kabisa," alisema.

Kuhusu masharti ya dhamana, Jaji Juma alisema wanapendekeza yalegezwe, akieleza kuwa wananchi wengi sasa wana vitambulisho vya taifa, hivyo kuna haja vitumike kama dhamana badala ya kumtaka mwananchi kuonyesha mali.

Alisema msongamano uliopo umetokana na upungufu katika sheria za nchi, akibainisha wengi wa wanaonyimwa dhamana ni wanaotuhumiwa kwa kesi kubwa zikiwamo za mauaji, uhujumu uchumi, dawa za kulevya na ubakaji.

“Kwa bahati mbaya kesi hizo zina adhabu kubwa na vilevile upelelezi unachelewa kukamilika, nadhani watu wa kulaumiwa hasa ni wapelelezi, siyo mahakama na wala siyo mtu mwingine, upelelezi unachukua muda mrefu na sababu wanazozitoa mahakamani kuhusu upelelezi kutokamilika, hazina mashiko," alisema.

Alisema kunapokuwa na kesi ya muda mrefu bila kukamilika kwa upelelezi, sheria inatakiwa kutamka wazi kwamba inapofika wakati fulani kama kesi haijakamilisha upelelezi wake, ifutwe.

“Sheria inatakiwa kutamka, sisi wa mahakama tutaitekeleza,” Jaji Mkuu alisema.

Kiongozi huyo wa mahakama pia aliwataka wananchi kubadilisha mtazamo wa kupenda adhabu kali zaidi badala ya kutoa adhabu mbadala.

“Ukisikiliza mijadala ya bungeni, kila mtu anataka adhabu kali miaka 30 ama 15, hizo zote zinachangia magereza kujaa," alisema.Aliongeza kuwa hata kwenye siasa za nchi nako kuna changamoto zinazopaswa kuangaliwa.

"Mkandarasi akishindwa kutekeleza matakwa ya mkataba, utasikia kamata weka ndani, hizi zote zinachangia, tuache masuala ya kijinai yaende kijinai na masuala yanayohusu mambo ya mikataba yaende kimkataba," alishauri.