Jaji Mkuu ataka Polisi iongezwe

17Apr 2018
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Jaji Mkuu ataka Polisi iongezwe

JAJI Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma ameshauri Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), kutumia uzoefu na ubunifu wake kuunganisha taasisi nyingine za utoaji haki nchini, ikiweno Jeshi la Polisi, kuwa sehemu ya mpango mkakati wa miaka mitano wa Mahakama nchini unaotekelezwa sasa.

JAJI Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma.

Mbali na Polisi, Prof. Juma ameishauri IJA kuziunganisha na Mahakama pia Jeshi la Wananchi (JWTZ) na Magereza.  

Jaji Mkuu alitoa rai hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa wadau wa kujadili ulinganisho wa IJA na vyuo vingine vya mafunzo endelevu vya ndani ya nchi.

"Mkutano huu unalenga kila taasisi inayotoa mafunzo itaweka mezani mambo mbalimbali kuhusu mafunzo endelevu ili kulinganisha na kutambua maeneo ya ushirikiano kati ya vyuo vya umma na vinavyotoa mafunzo endelevu," alisema Prof. Juma na kueleza zaidi:"Natambua mtapata nafasi ya kujadiliana kuhusu changamoto mbalimbali ikiwamo ulinganisho wa mafunzo endelevu.

"Kwa muda mrefu dhana hii ya ulinganisho imetumika na kufahamika zaidi katika nyanja za biashara na uwekezaji... sasa ni wakati muafaka wa IJA kuwaonyesha wadau wengine wa mafunzo endelevu uzoefu wake katika kutayarisha mpango wa mafunzo wa mahakama uliotayarishwa kwa misingi shirikishi."

Akifafanua zaidi, Prof. Juma alisema mahitaji ya huduma ya sheria na utoaji haki katika karne ya 21 ni tofauti na husukumwa na nguvu ya tehama na ushindani, na kwamba mafunzo yalenge mlinganisho utakaokidhi mahitaji ya karne hiyo.

Naye mwenyekiti wa bodi ya IJA, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani, John Mroso alisema mahakama ilianzisha chuo hicho kwa lengo la kuboresha na kuimarisha mafunzo bora kwa mhimili huo.

Habari Kubwa