Jaji Mkuu atoa angalizo ulipaji wa fedha uhujumu

09Oct 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Jaji Mkuu atoa angalizo ulipaji wa fedha uhujumu

JAJI Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahimu Juma, amesema suala la watuhumiwa kukiri na kulipa fedha linapaswa kufanyika kwa hiyari ili kukwepa watu kukimbilia Mahakama Kuu au Rufani.

JAJI Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahimu Juma, picha mtandao

Aidha, amesema jambo hilo ni zuri na siyo geni kufanyika Tanzania bata, huku akitoa mfano kuwa linatekelezwa Zanzibar, Kenya na Marekani.

Jaji Mkuu aliyasema hayo jana alipokutana na uongozi wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, tawi la Tanzania (Misa Tan), kujadili maeneo ya ushirikiano katika kuimarisha utoaji na upatikanaji wa taarifa kwa umma.

“Sheria ya kukiri makosa inasisitiza hiyari, Mahakama zinatakiwa kwamba makubaliano yaliyofanyika ni hiyari, kwa kuwa ikikosekana hiyari mapema ikifika Mahakama Kuu au Rufani ni tatizo,” alisema.

Alisema wananchi wanapaswa kuelimishwa uzuri wa jambo hilo, na kwamba kamati ya kanuni ya Jaji Mkuu ilipendekeza jambo hilo tangu mwaka 2013 na walitengeneza nyaraka.

“Ni jambo zuri sana na muhimu, linasaidia kupunguza msongamano magerezani, msongamano wa upelelezi, inasaidia wananchi kuwa wakweli… kama umefanya kosa unakuwa mkweli,” alisema na kuongeza:

“Nchi nyingine ni tofauti sana kwa kuwa Ulaya kuna chombo cha upelelezi cha kupima ukweli kinachoonyesha anayedanganya na kusema ukweli, imepunguza upelelezi.”

“Siku zote suala hili linapokuja linakutana na upinzani, maana hata Marekani walikataa na baadaye ikafanikiwa, hili jambo jema tusipoliripoti vizuri likaeleweka linaweza kuonekana siyo kitu kizuri na kujikuta inaondolewa kwa sababu ya namna ya uelewa wake,” alisema.

Jaji Juma alisema sheria inazungumzia suala hilo katika mahakama zote na wote wanaohusika na Mahakama, na kwamba ni nchi nzima na siyo sehemu ndogo ya jamii.

Wanahabari watumie sheria
Kadhalika, aliwataka waandishi wa habari kutumia nguvu ya kisheria kudai taarifa kwa kuwa imewekwa kwenye sheria ya upatikanaji wa taarifa ya mwaka 2016.

“Kwa bahati mbaya hizi nguvu hazitumiki, tumebaki kuomba kama ni fadhila badala ya kutumia nguvu za kisheria kudai kwamba sheria imekupa nguvu kwa taasisi yako kupata taarifa,” alisema.

Aidha, alisema sheria hiyo inatoa shuruti kwa taasisi kuwa lazima watoe taarifa zinazotakiwa na umma, na kwamba hakuna namna ya kukataa kutoa taarifa.

“Sheria ilivyotamka hivyo inaipa nguvu tamko la kikatiba, nyinyi mmepewa nguvu zaidi badala ya kutegemea zidi fadhila na kuomba…ni namna gani utatumia sheria kushurutisha ili habari zitoke,” alisema Jaji Juma.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, watumishi wa umma wanawajibika kuhakikisha taarifa mbalimbali zinakuwapo wakati wote ili wananchi au waandishi wasipate shida kuzipata.

Jaji Mkuu alisema kuwa Mahakama inafanyakazi katika mazingira ya uwazi na kuruhusu kukosolewa kwenye hukumu zake mbalimbali, ilimradi asikosolewe Jaji.

Awali, Mwenyekiti wa Misa-Tan, Salome Kitomari, alisema ushirikiano kati ya taasisi hiyo na Mahakama ulianza baada ya utafiti wa upataji taarifa wa mwaka 2014 kwa Mahakama kupata kufuli la dhahabu kutokana na kufungia taarifa.

“Mahakama chini ya Jaji Mkuu wa wakati huo, Othman Chande, ililichukua kufuli hilo kama fursa ya kufungua uhusiano na Misa Tanzania. Kuanzia wakati huo, mafunzo ya huduma bora kwa mteja na upataji taarifa kwa watumishi wa Mahakama na hadi Mei mwaka huu watumishi 300 wa kanda tofauti wamenufaika,” alisema.

Kitomari aliwataja wanufaika ni makarani, watunza kumbukumbu, watumishi wa mapokezi, makatibu mahsusi, walinzi na mahakimu wa mahakama za mwanzo na maafisa waajiri na tathmini ilionyesha kuna mabadiliko makubwa katika huduma kwa wateja.

Habari Kubwa