Jaji Mkuu awafunda Mahakimu Wakazi kutenda haki

18Jan 2022
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Jaji Mkuu awafunda Mahakimu Wakazi kutenda haki

JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, amewataka Mahakimu Wakazi wapya 29 wa Mahakama za Mwanzo, kuzingatia kanuni na kusimamia haki bila kujali kupokea maelekezo kutoka kwa mtu yeyote akiwamo yeye.

Kadhalika amesema, ikitokea Jaji Mkuu akapiga simu kuelekeza jinsi ya kutoa hukumu ya kesi fulani, haraka hakimu mhusika akatoe taarifa Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Jaji Mkuu alitoa rai hiyo jana katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki, jijini Dar es Salaam, wakati akiwaapisha mahakimu hao.

“Kazi ya Mahakimu na sisi majaji ni kufanyakazi kwa kuzingatia kanuni zetu, ikitokea hakimu unapigiwa simu na Jaji Mkuu akikuelekeza utoaji wa hukumu kesi unayoisikiliza, mara moja katoe taarifa Tume ya Utumishi wa Mahakama," alisisitiza Jaji Mkuu.

Akifafanua zaidi alisema misingi ya mahakimu ni kutenda haki kupitia ngazi mbalimbali, wakikosea wanakosea mfumo mzima wa utoaji haki.

"Ninyi ni matunda ya wazazi wenu na hazina ya taifa letu, miaka 25 ijayo mtashika nyadhifa mbalimbali za uongozi wa Mahakama Tanzania, lazima muelewe sheria na taratibu za utoaji haki," alisema Jaji Mkuu.

Aidha, alisema mahakimu na majaji wanamamlaka ya mwisho katika utoaji haki ambayo huanzia ngazi ya polisi pale mwananchi anapokwenda kutoa taarifa, upelelezi, kwa waendesha mashtaka Mahakama ya Mwanzo hadi Mahakama ya Rufani.

Naye Jaji Kiongozi, Mustapha Siyani, aliwataka wakatende haki kwa kufuata sheria na taratibu za mahakama kwa kuwa ni mhimili unaoaminika na kuwasihi wasiutie doa kwa vitendo vya rushwa.

Alisema kwa ukubwa na thamani ya kazi waliyopewa na taifa, waende wakachape kazi kwa juhudi na uadilifu na wakaijenge mahakama kwa kusimamia haki.

Habari Kubwa