Jaji Mkuu awafunda mawakili wapya

11Jul 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Jaji Mkuu awafunda mawakili wapya

JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, amewataka mawakili wapya 601 wa kujitegemea, kujihusisha na shughuli zingine za kiuchumi ikiwamo kilimo na ufugaji badala ya kutegemea kazi ya uwakili pekee.

Pia amewataka kuisoma Dira ya Taifa ya Maendeleo inayoeleza kwamba karne ya 21 ni ya ushindani.

Prof. Juma alitoa rai hiyo jana katika viunga vya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakati akiwapokea na kuwakubali kwa njia ya video mawakili hao waliokuwa wakifuatilia matangazo ya moja kwa moja kupitia Televisheni ya Taifa.

"Wengi hawajui Dira ya Taifa ya Maendeleo, wengi niliongea nao walisema hawajui dira inaelekea wapi, nawashauri ninyi mawakili mkajihusishe na shughuli za kiuchumi ikiwamo kilimo, mifugo na biashara badala ya kutegemea kazi ya uwakili pekee," alisema Prof. Juma.

Alisema pamoja na kujihusisha na shughuli za kiuchumi, ili kuendana na soko la ushindani, ni lazima wajikite kwenye matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TAHAMA) kwa kuwa mahakama inaandaa kanuni zitakazoanzisha mfumo wa kusajili kesi mbalimbali na kusikiliza kwa njia ya mtandao.

Alisema mawakili wengi bado wanakosa kazi za kudumu kutoka kampuni mbalimbali za uwakili, taasisi za umma na serikali kwa sababu kazi za kiwakili zimepungua kwa kuwa dunia ya sasa ya teknolojia ni ya kujichanganya katika fursa mbalimbali.

Jaji Mkuu alisema kipindi cha miezi mitatu ya kujilinda na virusi vya homa ya mapafu ya corona, mahakama nchini imesikiliza kesi 3,874 kwa njia ya mtandao wakati mahabusi wakiwa katika magereza husika.

Kuhusu maadili, Jaji Mkuu alisema mawakili hawana budi kuheshimu usiri kati yao na wahitaji wa huduma ya kufatuta haki ikiwamo kutunza siri bila kusahau kujifunza taaluma zingine.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Prof. Adeladus Kilangi, aliwaasa mawakili hao kuacha kujihusisha na vitendo vya kughushi nyaraka ikiwamo za mirathi kwa kuwa wajibu wao ni kusimamia haki kwa jamii.

Alisema tume ya maadili imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kuhusu mawakili kujihusisha na jinai kwa makusudi hali inayosababisha jamii kukosa imani nao.

Kwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk. Lugemeleza Nshala, alisema hiyo ni awamu ya 62 na ya kwanza ya mawakili 601 kuapishwa kwa njia ya mtandao na kwamba kikubwa ni kuyazingatia na kuyafanyia kazi maarifa waliyopewa.

Alisema majukumu yao kama mawakili ni kusimamia haki na kwamba bila nchi kuendeshwa kwa misingi ya sheria kumekuwa na uonevu mkubwa katika jamii.

Habari Kubwa