Jaji Mutunga atunga kitabu cha maisha ya ujaji mkuu

02May 2022
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam
Nipashe
Jaji Mutunga atunga kitabu cha maisha ya ujaji mkuu
  • Awataka Watanzania wakitumie kudai katiba mpya

JAJI Mkuu mstaafu wa Kenya, Willy Mutunga ameandika kitabu kuhusu aliyoyapitia akiwa kwenye nafasi hiyo, huku akiwataka watanzania kukisoma ili wapate mambo yatakayowasaidia kudai Katiba mpya.

Jaji Mutuga kwenye kitabu hicho ameelezea mchakato wote uliofanyika hadi nchi hiyo kufanikiwa kuwa na Mahakama Huru ambayo haiingiliwi na mhimili wowote kwenye kufanya maamuzi yake.

Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho alichokipa jina la Beacons of Judiciary Transformation, ambapo mgeni rasmi alikuwa Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Othman Chande.

Jaji Mutunga alikuwa Jaji Mkuu wa Kenya kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2011 mpaka 2016 na atakumbukwa na wakenya alivyoifanya Mahakama nchini humo kuwa huru katika maamuzi yake.

“Tanzania mnapambania katiba mpya na kuna ile rasimu ya Katiba ya Warioba kwa hiyo naona hiki kitabu kitawasaidia kwenye hayo mapambano kwa sababu kina mambo mengi kuhusu katiba mpya. Kitabu kinazungumzia shida za kupata hiyo katiba mpya na namna ya kuitekeleza,” alisema Jaji Mutunga.

Hata hivyo, Jaji Mutunga alisema kupata Katiba mpya ni kitu kingine na kuitekeleza ni kitu kingine kwani kwenye baadhi ya nchi uzoefu unaonyesha kuwa uzingatiaji wa Katiba unategemea matakwa ya Rais aliyeko madarakani.

“Kutekeleza Katiba kwenye baadhi ya nchi inakuwa ni mapambano mengine, Katiba ni nyaraka tu hivyo kuitekeleza kunaweza kuleta shida sana na mfano mzuri wa kiongozi wa kuigwa kwenye kutekeleza Katiba ni Mwalimu Julius Nyerere, lakini wengine ni shida sana,” alisema Mutunga.

 Kwa upande wake, Jaji Mkuu mstaafu, Othman Chande, alisema kitabu hicho nikumbukumbu ya hotuba 60 na maamuzi yake saba aliyoyatoa akiwa kwenye nafasi ya Jaji Mkuu wa Kenya kwa miaka mitano.

Alisema kwenye kitabu hicho Mutunga amejikita zaidi kwenye mageuzi ya mahakama ambapo baada ya kupata Katiba mpya mwaka 2010, wakenya wengi walitaka mahakimu na majaji wote afukuzwe kazi mahakama zote zifutwe waanze upya.

“Wakenya si kwamba tu walitaka Katiba mpya bali na mahakama mpya na yeye Mutunga ndiye alikuwa Jaji Mkuu wa kwanza ndani ya Katiba mpya ya Kenya alifanya mageuzi makubwa sana,” alisema.

Aidha, alisema Mutunga aliwezesha mahakama kuwa huru kutoingiliwa na mhimili mwingine na alikuwa Mwenyekiti wa Jopo la Majaji sita kwenye kesi ya kwanza ya uchaguzi wa urais mwaka 2013.

“Amezungumzia uzoefu wake kwenye hali kama hiyo, anasema katika kutoa uamuzi wa kesi za urais mara zote utafurahisha watu wa upande mmoja na utawaudhi watu upande mwingine lakini unapaswa kutoa uamuzi wa haki, “ alisema.

“Kwenye ile kesi aliamua kwamba Uhuru ndiye mshindi ingawa kuna watu walikuwa na matarajio  mengine na walimuona kama adui, lakini cha kutia moyo ni kwamba mwenyewe amesema kuwa wakati anamuapisha Uhuru Kenyatta alishangiliwa yeye zaidi wakati anaingia uwanjani kuliko hata huyo Rais mwenyewe,” alisema Chande.

 
 

Habari Kubwa