Jaji Mutungi ataka subira hatima ACT

19Apr 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Jaji Mutungi ataka subira hatima ACT

MSAJILI wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ametaka pawapo na subira kuhusu hatima ya chama cha ACT-Wazalendo kufutiwa usajili ama la na kuwa ofisi hiyo itatoa taarifa itakapokuwa tayari.

MSAJILI wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.

Akijibu swali la mwandishi wa gazeti hili aliyetaka kufahamu hatima ya chama hicho, Jaji huyo alisema ofisi hiyo haifanyi kazi kwa kushinikizwa, na kwamba itatoa majibu pale itakapokuwa tayari kufanya hivyo.

“Unauliza sasa ili iweje…tutatoa taarifa itakapo kuwa tayari,” alisema Jaji Mutungi alipoulizwa jana.

Machi 25 ofisi hiyo ilieleza nia yake ya kutaka kukifutia usajili chama hicho na kukipa siku 14 kuanzia Machi 26, kuwasilisha maelezo ya kwanini kisifutiwe unachama wa kudumu.

Hatua hiyo ilichukuliwa ikiwa imepita wiki moja tangu aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kujiunga na ACT-Wazalendo pamoja na waliokuwa viongozi waandamizi wa chama hicho na wanachama wa kawaida.

Msajili aliiandikia barua ACT-Wazalendo yenye kumbukumbu namba HA.322/362/20/98 ya Machi 25, mwaka huu, kujieleza kwanini isifutiwe usajili wa kudumu kwa vitendo vya uvunjifu wa sheria ikiwamo kutowasilisha hesabu za ukaguzi mwaka 2013/14.

Chama hicho pia kinadaiwa kuchoma moto bendera za CUF baada ya mahakama kutoa hukumu iliyompa uhalali Prof. Ibrahimu Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa CUF.

Barua hiyo pia imekituhumu chama hicho kutumia dini katika siasa zake baada ya mashabiki kuonekana katika mitandao wakipandisha bendera yao kwa kutumia tamko takatifu la dini ya kiislam (Takbiir), kitendo ambacho Ofisi ya Msajili inasema imekiuka kifungu cha 9(1)c ya Sheria ya Vyama vya Siasa.

Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, alinukuliwa na vyombo vya habari akidai chama hicho kimewasilisha barua ya maelezo yenye majibu ya hoja walizoulizwa na Msajili.

Habari Kubwa