Jalada kesi vigogo almasi latua kwa DPP

14Feb 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Jalada kesi vigogo almasi latua kwa DPP

JALADA la kesi ya uhujumu uchumi ikiwamo kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 2.4 inayomkabili Mkurugenzi wa Tathmini ya Madini, Archard Kalugendo, liko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa ajili ya  uchunguzi.

Mbali na Kalugendo, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni, Mthamini wa Madini ya Almasi wa Serikali, Edward Rweyemamu.

Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa.

Wakili wa Serikali, Esterzia Wilson, alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba jalada la kesi hiyo liko kwa DPP kwa hatua za kiofisi.

Hakimu Mwambapa alisema Hakimu Mkazi Mkuu Respicius Mwijage yuko likizo, hivyo washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu na kesi hiyo itatajwa tena Februari 27, mwaka huu. 

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kuisababisha serikali hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 2.4.

Ilidaiwa kuwa kati ya Agosti 25 na 31, 2017 katika maeneo mbalimbali kati ya Dar es Salaam na Shinyanga, kwa pamoja na kwa vitendo vyao wakiwa wathamini walioajiriwa na Wizara ya Nishati na Madini waliisababisha serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha.

 

Habari Kubwa