Jamhuri yaomba kesi uhujumu uchumi kuahirishwa siku 14

18Jul 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Jamhuri yaomba kesi uhujumu uchumi kuahirishwa siku 14

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kutakatisha fedha inayowakabili vigogo wa Kampuni ya Six Telecoms, akiwamo wakili mwandamizi wa kujitegemea, Dk. Ringo Tenga na wenzake, umeiomba mahakama kuahirisha kesi ndani ya siku 14 kwa kuwa wanaandaa nyaraka muhimu.

Ringo Tenga na wenzake.

Madai hayo yalitolewa jana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Hakimu alisema kesi hiyo itatajwa Julai 26, mwaka huu.

Aprili 5, mwaka huu upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

"Mheshimiwa hakimu kesi hii imepangwa kwa ajili ya kutajwa na Jamhuri tunaifahamisha mahakama kwamba upelelezi wake umekamilika tunaandaa nyaraka kwa ajili ya kuanza mchakato wa kusikilizwa,” ulidai upande wa Jamhuri.

Mbali na Dk. Tenga, washtakiwa wengine ni Mhandisi na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Hafidhi Shamte maarufu Rashidi Shamte, mfanyabiashara na mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni, Mkuu wa fedha wa kampuni hiyo Noel Chacha na kampuni ya Six Telecoms Limited wanadaiwa kutakatisha Sh. Bilioni nane.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya utakatishaji wa fedha, hivyo kuwafanya wasote mahabusu kwa kuwa makosa hayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Habari Kubwa