Jamhuri yatwishwa zigo kumamatwa Lissu

22Feb 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Jamhuri yatwishwa zigo kumamatwa Lissu

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imetoa siku 14 kwa upande wa Jamhuri kujibu maombi ya wadhamini wa Mbunge wa zamani Singida Mashariki, Tundu Lissu, kwamba wameshindwa kumpata ili mahakama itoe amri ya kumkamata.

Wadhamini hao, Robart Katula na Ibrahim Ahmed, kwa nyakati tofauti jana waliieleza mahakama kuwa wamewasilisha maombi wakiomba mahakama itoe hati ya kukamatwa kwake ili wajitoe udhamini kutokana na mtuhumiwa huyo kutohudhuria kesi yake.

Amri hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, baada ya upande wa Jamhuri kukiri kupokea maombi hayo na kwamba wanaomba muda wa kuyajibu.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa upande wa Jamhuri umepokea maombi yaliyoambatanishwa na hati ya kiapo lakini wanaomba muda wa kutosha kuyachambua.

Hakimu Simba alisema mahakama yake inatoa siku 14 kwa upande wa Jamhuri na kuwasisitiza watumie siku 10 kuhakiki maombi hayo kabla ya kurejea mahakamani.

Katika kesi ya msingi, Hakimu Simba, aliwataka wadhamini kueleza alipo mshtakiwa Lissu kwa kuwa walishakiri kwamba amepona na mahakama ilihitaji kumwona akihudhuria kesi.

Mmoja wa wadhamini hao, Katula, alidai kuwa ni kweli alisema mshtakiwa amepona lakini walipojaribu kuwasiliana naye ili aje mahakamani alidai ana wasiwasi na usalama wa maisha yake ndiyo maana ameomba mahakama ishughulikie maombi yao.

Kabla ya hakimu kupanga tarehe, Wakili Simon alidai kuwa mshtakiwa namba mbili katika kesi hiyo, Simon Mkina, hakuonekana mahakamani kwa siku mbili bila taarifa, hivyo akaiomba mahakama itakaporudi mshtakiwa aonywe na wadhamini wake watoe maelezo ni kwa nini mshtakiwa hakuhudhuria mahakamani.

Akijibu hoja hiyo Wakili wa Utetezi, Nyaronyo Kicheere, alidai kuwa jana Mkina alifika lakini aliumwa ghafla akalazimika kurudi nyumbani na bado hali yake si nzuri.

Hakimu Simba aliendelea kusisitiza wadhamini wa Lissu kumleta mahakamani hapo kwa kuwa amri za kesi hiyo bado zinaendelea mpaka zitakapotenguliwa baadaye. Kesi hiyo imeahirishwa mpaka Machi 10, 2020.

Lissu na wenzake wanne katika kesi ya msingi wanakabiliwa na mashtaka matano ikiwamo kuandika habari za uchochezi kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.

Ilidaiwa kuwa kati ya Januari 12 hadi 14, 2016 jijini Dar es Salaam, washtakiwa Jabir Idrisa, Mkina na Lissu, waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar.’

Katika shtaka la pili, wanadaiwa kuwa Januari 14, 2016 walichapisha habari hizo ili kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar.

Mshtakiwa Mehboob anadaiwa kuwa Januari 13, 2016 katika jengo la Jamana lililopo Manispaa ya Ilala, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa huyo pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya sheria ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Habari Kubwa