Jamii ya endelea kupewa elimu kuhusu Uviko 19

14Oct 2021
Zanura Mollel
Longido
Nipashe
Jamii ya endelea kupewa elimu kuhusu Uviko 19

​​​​​​​KASI ya kuendelea kutoa chanjo ya ugonjwa wa Uviko 19 wilayani Longido mkoani Arusha inaendelea kwa kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa chanjo hiyo kabla ya kuwachanja.

Nurudin Babu.

Akizungumza na wafanyabiashara, Mkuu wa Wilaya hiyo Nurudin Babu, amewasahuri kuchanja chanjo hiyo ili waweze kujilinda na ugonjwa huo lakini pia kuepuka maambukizi wakati wanapo ihudumia jamii.

Amesema serikali ilitoa chanjo 2,790 kwa Wilaya hiyo pamoja na kuwa jamii ilikua na ugumu wa kukubali kuchanjwa lakini tuliendela kutoa elimu na wakakubali kuchanja, hivyo Wilaya hiyo imefanikiwa kuchanja kwa asilimia 100.

"Niwaambie ukweli chanjo kwa sasa wilayani imeisha, endeleni kufuata taratibu za kiafya kunawa mikono na kutumia vitakasa mkono pamoja na kuvaa barakoa" amesema DC Babu.

Akitolea mfano kata ya Mundarara ambayo ni kata yenye machimbo ya madini aina ya Vito (Rubi) amesema kuna watu zaidi ya 2,000 na wamesongamana wanatafuta madini hapo lakini wamekua wazito kukubali kuchanja.

"Nimewapa elimu nikawaambia mkachanje wakasema wanatumia miti shamba (dawa za asili)" amesema Babu.

Hata hivyo Mganga Mkuu wa Wilaya Dk. Seleman Mtenjela, amesema chanjo ya Uviko 19 imejaribiwa kupitia tafiti mbalimbali kisayansi na imethibitishwa na shirika la afya duniani (WHO) nakuidhinishwa na Wizara ya Afya kupitia mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA), hivyo ni salama.

"Ni aina nne zimeaidhinishwa kutumika hapa nchini kwa ajili ya kinga ya Uviko 19 ambazo ni Johnson& Johnson, Pfizer,Moderna na Sinovac &Sinopharm" amesema Mtenjela.

Aidha, amefafanua kuwa pamoja na kupata chanjo unashauriwa kuendelea kujikinga na Uviko 19 kwa kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabauni au kutumia kitakasa mkono, kuepuka misongamano, kufanya mazoezi na kuzingatia lishe bora.

Naye, Mzee wa mila Thomas Ole Ngulupa, ametoa ushuhuda juu ya chanjo hiyo amesema amechoma chanjo hiyo na wake zake wanne na hadi sasa hajapata maradhi wala misukosuko yoyote kupitia chanjo hiyo.

"Niko salama na wake zangu wapo salama pia, niombe serikali iendelee kuelimisha jamii yetu kuipokea chanjo vizuri" amesema Ole Ngulupa.