Jamii yaonyeshwa fursa utalii Iringa

14Sep 2021
Christina Haule
Iringa
Nipashe
Jamii yaonyeshwa fursa utalii Iringa

JAMII imetakiwa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini, likiwamo eneo la Kikongoma lenye historia ya mwanamama jasiri mkoani Iringa.

Mwanamke huyo aliona bora kujiua kuliko kuchukuliwa na maadui au kutaja siri za mwanae Chifu Mkwawa wakati wa mapigano na Wajerumani kweye miaka ya 1880.

Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na kundi la wanahabari wanawake 31 waliotembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, kwa lengo la kutangaza na kuhamasisha utalii na uwekezaji nchini.

Alisema mwanamama huyo ambaye ni mama yake Chifu Mkwawa aliamua kujitumbukiza kwenye maji yaliyozungukwa na jiwe, huku kukiwa na tundu dogo la jiwe na kufariki dunia ili kuzuia asitekwe na maadui waliomtaka kutoa siri za Mkwawa.

“Historia hiyo imebeba ujasiri mkubwa kwa wamama, sababu mwanamke huyo alionyesha ujasiri na thamani ya mwanamke kwa kuamua kutoa roho yake kuliko kumwangamiza mwanawe kwa kutoa siri zake … ninyi kama wanahabari wanawake na jamii kwa ujumla mnayo nafasi ya kufika na kujifunza,” alisema.

Ngwada alisema Iringa ni mkoa wa kishujaa kwa sababu ya historia ya Chifu Mkwawa, ambaye alipigana vita kubwa kwa kutumia silaha za jadi na wenzake kwa kutumia silaha za moto, lakini yeye Mkwawa aliwashinda ambapo historia hiyo kubwa ipo makumbusho ya Karenga.