Jamii yatakiwa kuacha kumaliza kesi za ukatili nyumbani

04Jul 2022
Beatrice Shayo
Nipashe
Jamii yatakiwa kuacha kumaliza kesi za ukatili nyumbani

WANANCHI wameshauriwa kuhakikisha wanaacha mchezo wa kumaliza kesi katika ngazi ya familia kwani inasababisa madhara makubwa kwa wahusika waliotendewa ukatili.

Hayo yalisemwa jana jijini na Ofisa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maaalum, Baraka Lucas katika maonyesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITE) katika viwanja vya Sabasaba.

Lucas alisema kuna kesi ambazo zinamazilika kirafiki ama katika ngazi ya jamii hasa katika matendo ya ukatili jambo ambalo sio sahihi.

“Kimsingi mtu yoyote hata kama ni ndugu yako ama jirani ametenda kosa hilo ni kosa kinachovunjwa pale ni sheria na haki ya mtu weka urafiki mbali na undugu angalia haki ya mtu,”alisema Lucas

Lucas alisema wao kama serikali wanasisitiza kuwa watu wasimalizane kesi katika ngazi ya familia zipo sheria ambazo nchi inazitumia kusimamia haki za kila mwanadamu.

Alisema jamii inapotokea imebaini tatizo hilo ni vyema ikawasilisha taarifa rasmi kwenye mamlaka hususani jeshi la polisi, vituo vya afya na mamlaka za sheria ikiwemo mahakama ili mashauri hayo yaweze kusikilizwa.

“Kumaliza kesi hizo katika ngazi ya familia kuna athari kubwa kwa mtendewa wa kosa na kwa mtenda kosa. Mtendewa kosa anakwenda kuathirika anapoona yule aliyemfanyia tendo la ukatili bado yupo mtaani maana yake anaweza kupoteza amani ama kujizuru ama akaenda kumzuru aliyemtendea ubaya,” alisema

Lucas alisema kuna jambo jingine la kuangalia kwa upande wa jamii itajifunza kitu gani kama mtu amefanya kosa katika mazingira ambayo ameshuhudiwa ina maana hakuna umuhimu wa kuwepo kwa mifumo ya kisheria katika nchi.

“Ni rai yangu watu wapaze sauti zao nasisitiza watumie mifumo ambayo ipo katika jamii ili kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili wale wanaotenda makosa waweze kuwajibishwa kwa sababu watu hao wanafanya makosa ya jinai na sheria zipo za nchi zinazoweza kuwaajibisha na sio kumalizana katika ngazi ya familia kwa sababu ya undugu ama urafiki mwisho wa siku wanavunja misingi ya haki za binadamu,”alisema Lucas.

Habari Kubwa