Jamii yatakiwa kuwashirikisha wenye ulemavu

06Dec 2019
Na Mwandishi Wetu
Kilimanjaro
Nipashe
Jamii yatakiwa kuwashirikisha wenye ulemavu

WATANZANIA wametakiwa kuimarisha utamaduni wa kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika kazi mbalimbali kwani wanao uwezo iwapo watapewa fursa.

Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na vijana, Tanzania Youth Coalition (TYC), Lenin Kazoba

Wito huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Tanzania Youth Coalition (TYC), Lenin Kazoba, katika kongamano linalofanyika Weruweru, wilayani Hai, Kilimanjaro likishirikisha vijana 60 kutoka nchi tano za Afrika Mashariki za Tanzania, Rwanda, Kenya, Uganda na Burundi.

Kongamano hilo linalenga kuwajengea uwezo vijana katika maeneo mbalimbali ili waweze kuwa washiriki wenye tija katika kufikia maendeleo endelevu ya nchi zao na eneo la Afrika Mashariki.

TYC ni mwamvuli wa mashirika yasiyo ya kiserikali na vyama vya kijamii zaidi ya 120, vinavyohusika na maendeleo ya vijana katika nyanja mbalimbali Tanzania Bara na Visiwani.

“Ni muhimu tuangalie namna ya kuwapa fursa zaidi, kuwatia moyo na kuwajengea uwezo watu wenye ulemavu,” alisema Kazoba wakati wa kutambua Siku ya Walemavu Duniani inayoadhimishwa kila mwaka Desemba 3.

Mmoja wa washiriki, Lilian Munuo 23, alisema bado juhudi zinatakiwa kwa jamii kutambua mahitaji ya wenye ulemavu.

“Wakati mwingine watu hufikiria kuwa huwezi kufanya jambo fulani kwa kutotaka tu, huku ikiwa ni kweli una changamoto ya ulemavu. Hili huumiza,” alisema Lilian mwenye tatizo linalofahamika kitaalamu kama `muscular dystrophy` linalosababisha matatizo katika misuli na kuathiri utendaji kazi wa viungo.

Lilian ambaye ni mbunifu na mchoraji pia ametoa wito kwa serikali na mashirika binafsi kuendelea kuwafikiria walemavu wakati wote wa miradi ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali hapa nchini ili kuwa na mazingira rafiki kwao.

Naye Colman Ndetembea, alisema ni muhimu kuongeza juhudi kuwapatia watu wenye ulemavu wenye ulemavu vifaa saidizi, fursa na matibabu yanayotakiwa.

Colman alibuni kiti mwendo kinachoweza kusaidia walemavu au wagonjwa mbalimbali wa viungo kama waliovunjika uti wa mgongo na wenye matatizo ya misuli miongoni mwa wengine.

Chombo hicho kinaweza kikatumika kama kiti, kitanda au kumsaidia ambaye hawezi kusimama kufanya hivyo kama sehemu ya mazoezi.

Katibu Tawala Msaidizi (Utawala na Rasilimali Watu), Mkoa wa Kilimanjaro, Bwai Biseko, aliwataka vijana wanaoshiriki kongamano hilo kutumia maarifa watakayopata kuleta tija zaidi katika sekta za uzalishaji kama uvuvi, ufugaji wa wanyama, nyuki, samaki na misitu katika nchi zao.

“Hizi ndizo sekta zinazoweza kuwa na soko kubwa katika nchi zetu ni muhimu kwa vijana kufanya kazi kimkakati na jumuiya za ushirikiano wa kikanda Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Soko la pamoja la Mashariki, Kati na  na Kusini mwa Afrika (COMESA),”alisema.

Habari Kubwa