Jela maisha kwa kumlawiti mtoto

12Sep 2020
Jumbe Ismaily
Singida
Nipashe
Jela maisha kwa kumlawiti mtoto

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida imemhukumu kifungo cha maisha jela mkazi wa Mtaa wa Minga, Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Hussein Azizi (34), baada ya kukiri kosa la kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka minne.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi Robert Oguda, alisema anatoa adhabu kwa mshtakiwa ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Awali, Mwanasheria wa Serikali, Elizabeth Barabara, alidai kwamba mshtakiwa alitenda kosa la kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka minne, Agosti 6, mwaka huu, katika Mtaa wa Minga.

Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, mshtakiwa alidai kuwa watoto hao walikuwa wakimfuata hadi machungani kutokana na kuwa walimpenda sana na kwamba hakuwa amefanya tendo hilo mara moja bali alikuwa akifanya mara kwa mara.

Barabara alidai kuwa mshtakiwa huyo baada ya kusomewa shitaka lake hilo, alikiri kwamba hakuwa akifanya kitendo hicho kwa mtoto huyo peke yake bali kulikuwa na mtoto mwingine ambaye aliyefanya naye bila kugundulika.

Baada ya kusomewa mashtaka na kukiri na kabla ya kutiwa hatiani, mshtakiwa alijitetea kwa kuomba msamaha na kuahidi kwamba hatarudia tena kufanya kitendo kama hicho.

Pia katika utetezi wake, mshtakiwa alikiri kwamba kitendo alichokifanya kwa watoto hao wawili, hakikuwa kizuri, hivyo aliiomba mahakama imwonee huruma na kumpa adhabu ndogo.

Habari Kubwa