Jela maisha, miaka 60 na 30 kubaka wanafunzi na kulawiti

14Oct 2021
WAANDISHI WETU
Dar es Salaam
Nipashe
Jela maisha, miaka 60 na 30 kubaka wanafunzi na kulawiti

WATU watano, wakiwamo babu na mjukuu, wamehukumiwa vifungo vya maisha, miaka 60 na 30 jela baada ya kukutwa na makosa ya kubaka na kuwapa ujauzito wanafunzi pamoja na kulawiti.

Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya, dereva wa Bajaj, Deus Peter (25) Mkazi wa VETA jijini humo, amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumbaka na kumsababishia ujauzito mwanafunzi wa kidato cha nne, hivyo kukatisha masomo yake.

Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mkazi Andrew Scout, baada ya mshtakiwa kufikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka mawili na kukiri kutenda makosa hayo.

Akisoma mashtaka hayo katika kesi namba 59 ya mwaka 2021, Wakili wa Serikali, Hebel Kihaka akisaidiana na Zena James alidai kuwa kwa nyakati tofauti kati ya Septemba 2020 na Aprili 2021, mshtakiwa alimbaka mwanafunzi wa shule moja ya sekondari (jina la mwanafunzi na shule vinahifadhiwa) kinyume cha kifungu namba 130(1)(2)(e) na 131(1) cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Kosa la pili ni kijana huyo ni kumsababishia ujauzito mwanafunzi huyo kinyume cha kifungu cha 60 A (3) cha cha Sheria ya Elimu Sura ya 353.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo mawili, upande wa mashtaka uliiomba mahakama kutoa adhabu kama sheria inavyoelekeza ili iwe fundisho kwa mshtakiwa na watu wengine kwenye jamii.

Hata hivyo, mshtakiwa aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa kuwa bado ni kijana anayetegemewa na kosa hilo ni la kwanza na kwamba anajutia makosa hayo.

Baada ya maelezo ya pande zote, Hakimu Scout alimhukumu Peter kwenda kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kwanza na kosa la pili la kumsababishia ujauzito mwanafunzi huyo nalo atumikie kifungo cha miaka 30 jela. Hakimu alisema makosa hayo yanakwenda pamoja hivyo, atatumikia kifungo cha miaka 30.

Jijini Dar es Salaam, dereva Paul Vedastus, maarufu kama Majani (33), amehukumiwa kwenda jela miaka 60, baada ya kukutwa na hatia kumbaka na kumpa ujeuzito mwanafunzi.

Hukumu hiyo ilisomwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Hakimu alisema mahakama yake baada ya kusikiliza mashahidi wa pande zote mbili, bila kuacha shaka imemwona mshtakiwa ana hatia katika makosa yote mawili.

Alisema kosa la kumbaka mwanafunzi, mshtakiwa atakwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 30 na kosa la pili la kumpa mimba, pia atatumikia kifungo cha miaka 30 na adhabu zote zitakwenda sambamba.

Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mwanaamina Kombakono, alidai kuwa upande wa Jamhuri hauna kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya mshtakiwa, aliomba mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria.

Akitoa utetezi wake ili apunguziwe adhabu, mshtakiwa aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwa kuwa ana familia inamtegema.

“Mimi ni mzazi wa watoto watatu wote wanasoma na nina wazazi wananitegemea, wagonjwa, mama yangu anasumbuliwa na kansa ananitegemea mimi na pia baba yangu ni mwanajeshi mstaafu ambaye ameathirika na ugonjwa wa Ukimwi, wote wananitegemea mimi," mshtakiwa alisema akiomba huruma ya mahakama.

Hakimu Simba alisema adhabu ya makosa kama hayo imepangwa kwa mujibu wa sheria, kwasababu ya wanafunzi wanaopewa mimba na hakuna namna ya kuibadilisha ni miaka 30 jela kila kosa.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa, kati ya Mei na Agosti, 2016, eneo la Tandika wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam mshtakiwa alimbaka na kumpa mimba mwanafunzi.

Mkoani Singida, Mahakama ya Wilaya ya Singida, imemhukumu kifungo cha maisha jela, mkazi wa Mtaa wa Mizani,Kata ya Mandewa, mkoani Singida, Hamisi Shabani (25), kwa makosa ya kubaka na kulawiti.

Aidha, Mahakama hiyo pia imemhukumu adhabu ya kifungo cha nje cha mwaka mmoja, Shabani Rajabu (17), mkazi waa Mtaa wa Mizani, Manispaa ya Singida baada ya kumtia hatiani kwa makosa ya kubaka na kulawiti.

Rajabu amehukumiwa kifungo cha nje kutokana na kusimamiwa na sheria ya watoto kutokana na umri wake kutofikia miaka 18.

Hukumu ya kesi ya jinai namba 168/2020 ilitolewa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Robert Oguda, baada ya kusikiliza mashahidi saba ambao alisema ushahidi wao haukuacha shaka.

Ilidaiwa kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 27, mwaka jana, majira ya saa za usiku, mtaa wa Mizani, Kata ya Mandewa, Manispaa ya Singida ambapo washitakiwa huyo alikuwa akiishi nyumba moja na mwanamke huyo waliyembaka na kumlawiti.

Ilidaiwa mahakamani humo kuwa siku ya tukio walinunua pombe ya kienyeji na kumkaribisha mwanamke na kuanza kunywa pamoja hadi alipolewa, na kumfanyia kitendo hicho kwa zamu.

BABU NA MJUKUU

Mahakama ya Wilaya ya Chato, mkoani Geita, imewahukumu watu wawili kutumikia kifungo cha maisha jela kwa kosa la kumbaka mwanafunzi wa darasa la sita mwenye miaka 16 na kumsababishia maumivu makali.

Waliohukumiwa vifungo hivyo ni Fabiani Filipo (22) na Thomas James (48) wote ni wakazi wa Kijiji cha Kasala Wilaya ya Chato.

Hukumu hiyo imetolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Erick Kagimbo, baada ya ushahidi kuthibitisha kosa hilo pasipokuacha shaka yoyote na kuwatia hatiani washtakiwa hao.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Clemence Mango alipeleka mashahidi wanne na kielelezo kimoja ambavyo vilithibitisha kuwa washtakiwa hao walimbaka mwanafunzi huyo ambaye jina lake limehifadhiwa.

Akisoma huku hiyo, Hakimu Kagimbo alisema mshtakiwa wa pili Thomas James alimchukua mwanafunzi huyo na kumpeleka katika Kijiji cha Kasala, wilayani Chato kwa mjukuu wake ambaye ni mshtakiwa wa kwanza Fabiani Filipo kwa lengo la kumuozesha.

Aidha alisema baada ya kufika katika Kijiji cha Kasala mshtakiwa wa pili ambaye ni babu wa mshtakiwa wa kwanza alimkabidhi mjukuu wake mwanafunzi huyo na kuishi naye kama mke wake kuanzia mwenzi wa tatu hadi mwezi wa nane mwaka 2020.

Imeandikwa na Grace Mwakalinga (MBEYA), Hellen Mwango (DAR), Jumbe Ismailly (SINGIDA) na Joctan Ngelly (CHATO).

Habari Kubwa