Jela miaka 5 kwa wizi wa magodoro shuleni

24Nov 2020
Samson Chacha
Tarime
Nipashe
Jela miaka 5 kwa wizi wa magodoro shuleni

MKAZI wa Mtaa wa Serengeti Mjini Tarime mkoani Mara, Francis Chacha
Mokera (18), amehukumiwa kwenda jela miaka mitano baada ya kupatikana na
hatia ya kuvunja na kuiba mali za Shule ya Sekondari Tarime zenye
thamani ya Sh. 2,850,000.

Mahakama ilimkuta Chacha na hatia ya kuiba mali hizo ambazo ni magodoro, viti na taa za umeme.

Akisomewa hukumu hiyo katika kesi ya jinai namba 155/2020 Novemba 20, 2020,  Hakimu wa Mahakama ya Wilaya Tarime, Vicensia Balyahula, alisema kuwa ameridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka bila kuacha shaka yoyote.

Awali mwendesha  mashtaka wa Polisi, Thabiti Temba, alidai kuwa mshtakiwa alitenda wizi huo  kwa kuvunja milango ya Shule ya Sekondari Tarime  na kuiba  magodoro, viti vya chuma  na taa za umeme,  vyote vikiwa na thamani ya  kiasi hicho cha fedha kwa nyakati tofauti  katika kipindi cha Machi na Mei 2020
na kusababisha hasara kwa shule hiyo pamoja na wanafunzi kuathirika kimasomo.

Hakimu Vicensia alisema vitendo hivyo vya wizi, katika shule ni hujuma, hivyo nakuhukumu kwenda kutumikia kifungo cha miaka mitano jela ili iwe fundisho kwa watu wengine wanaohujumu mali za umma.

Habari Kubwa