Jela miaka 60 kwa unyang’anyi, ubakaji

23Mar 2017
Ahmed Makongo
MUSOMA
Nipashe
Jela miaka 60 kwa unyang’anyi, ubakaji

MAHAKAMA ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara, imemhukumu Joseph Nyakibore (22), mkazi wa mtaa wa Majengo mjini Musoma, kutumikia kifungo cha miaka 60 jela na kuchapwa viboko 24, baada ya kupatikana na hatia ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kubaka.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Musoma, Richard Maganga, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa.

Katika kosa la unyang’anyi alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kuchapwa viboko 24.

Viboko hivyo atachapwa 12 wakati wa kuingia gerezani na wakati wa kumaliza kifungo chake atamalizia 12.

Aidha, kosa la kubaka, mshtakiwa alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, pamoja na kumlipa mlalamikaji Shilingi milioni moja. Adhabu hizo zote zina jitegemea.

Awali ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Inspekta wa Polisi, Theophli Mazuge, kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo, Juni 7, mwaka jana.

Aliiambia mahakama siku ya tukio mshtakiwa akiwa na wenzake watano wakiwa na silaha, walivamia nyumba ya Daniel Mjalifu, mkazi wa mtaa huo na kupora vitu mbalimbali pamoja na kumbaka mwanamke mmoja.

Hata hivyo, alisema watu wengine wanne walifanikiwa kukimbia na kutokomea kusikojulikana.

Habari Kubwa