Jela miaka mitatu kwa kujeruhi

12Apr 2017
Jumbe Ismaily
IGUNGA
Nipashe
Jela miaka mitatu kwa kujeruhi

MAHAKAMA ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, imemhukumu Juma Maganga (34) mkazi wa kata ya Nkinga, wilayani hapa kifungo cha miaka mitatu jela baada ya kupatikana na hatia ya kujeruhi kwa kutumia spoku ya baiskeli.

Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Elimajidi Kweyamba, alidai juzi kuwa katika Novemba 12, mwaka jana saa tatu usiku, katika Kata ya Nkinga, mshtakiwa alimjeruhi kwa kumchoma jicho la kushoto mwalimu mstaafu Paschal Mwininga (67) kwa kutumia kifaa hicho chenye ncha kali.

Mbele ya Hakimu Mfawidhi Ajali Milanzi, Kweyamba alidai kwamba mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kinyume cha kifungu 225 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002.

Hata hivyo, baada ya mshtakiwa kusomewa mashtaka hayo, alikana kutenda kosa hilo na ndipo upande wa mashtaka ulipoamua kupeleka mashahidi wake wanne, akiwamo na mwathirika wa tukio hilo, ambao wote kwa pamoja walimtambua mtuhumiwa.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Milanzi alisema ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, umemwona mshtakiwa kuwa ana hatia, hivyo atakwenda gerezani kuanza kutumikia kifungo cha miaka mitatu, ili liwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Habari Kubwa