Jela mwaka kwa kumtukana Rais

22Sep 2016
Joctan Ngelly
Nipashe
Jela mwaka kwa kumtukana Rais

MKAZI wa Mlole Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Mshobozi Tibaigana (22), amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela ama kulipa faini ya Sh. 100,000 baada ya kupatikana na hatia ya kumtukana Rais John Magufuli.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma, Sylivester Kainda baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka kuthibitisha kosa hilo.

Hata hivyo, mshtakiwa alilipa faini hiyo na hivyo kuepuka kifungo.

Mshtakiwa alidaiwa kumtusi Rais Magufuli kwa maneno ambayo yanaleta uvunjifu wa amani.
Hakimu Kainda alisema mahakama hiyo inatoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wenye tabia kama yake.

Alisema upande wa mashtaka ulipeleka mahakamani hapo mashahidi wanne ambao walithibitisha kuwa mshtakiwa alimtukana Rais Magaufuli.

Awali ilidaiwa kuwa mshtakiwa alitoa matusi hayo akiwa ndani ya teksi yenye namba za usajili T 211 DGB, aliyokuwa amepewa 'lift' kutoka Buhigwe kwenda Mkatanga, wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.
Ilidaiwa kuwa gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Hamis Hussein, ambaye baada ya kusikia mshtakiwa akimtukana Rais Magufuli, alikwenda kutoa taarifa Kituo Kikuu cha Polisi mjini Kigoma na mtuhumiwa akakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Baada ya mahakama kumpa mshtakiwa nafasi ya kujitetea, aliangua kilio.
"Mheshimiwa Hakimu, naiomba mahakama yako tukufu inipunguzie adhabu kwa kuwa nina familia inayonitegemea. Pia ni kosa langu la kwanza.

Hata hivyo, Hakimu Kainda alitupilia mbali utetezi huo akisema: "Kwa kitendo chako ulichokifanya cha kumtukana Mkuu wa nchi matusi makubwa kama hayo, utakwenda jela mwaka mmoja au ulipe faini ya Sh. 100,000 ili iwe fundisho kwa watu wote wanaotukana viongozi wakuu."

Mshtakiwa alilipa faini hiyo baada ya ndugu zake kumchangia na hivyo kuachiwa huru.
Awali, Wakili wa Serikali, Shabani Masanja, alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Agosti 4, mwaka huu majira ya jioni eneo la Mkatanga Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.

Habari Kubwa