Jengo la Bunge Dodoma lakarabatiwa kwa mil. 912/-

26Feb 2016
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Jengo la Bunge Dodoma lakarabatiwa kwa mil. 912/-

JENGO la Bunge limeanza kufanyiwa ukarabati kutokana na baadhi ya maeneo kuvuja maji likiwamo paa la ukumbi wa Bunge.

Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Bunge, Owen Mwandumbya.

Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano Bunge, Owen Mwandumbya, alithibitisha jengo hilo kufanyiwa ukarabati huo na akieleza kwamba halijawahi kukarabatiwa tangu lijengwe takriban miaka 10 iliyopita.

Mwandumbya alisema kwa mujibu wa Wakala wa Majengo nchini (TBA) ambao ndiyo wasimamizi wa ukarabati huo, utagharimu Sh. milioni 912.

Alifafanua kuwa maeneo yatakayofanyiwa ukarabati huo ni pamoja na paa hilo ambalo kuna maeneo yalianza kuvuja maji na usingefanyika miundombinu mingine iliyopo ndani ya jengo hilo pia ingeharibika.

Alisema ukarabati huo utakwenda sambamba na kuongeza viti na meza 36 kwa ajili ya wabunge.

“Viti vilivyokuwapo vilikuwa ni 350, sasa hivi Bunge linatakiwa kuwa na wabunge takriban 396. Tunaongeza viti 36 mkandarasi yule yule aliyeweka viti ndiye atakayevileta hivyo na kuweka na kwa kuwa jengo linasimamiwa na Wakala wa Majengo, wao ndiyo wanaosimamia manunuzi ya viti hivyo,” alisema.

Alisema ukarabati mwingine ni kubadili meza zote za wabunge zilizokuwa zimeharibika ambazo asilimia kubwa zilikuwa zimechakaa na baadhi kuvunjika.

“Meza zote zitaondolewa na kuwekwa nyingine mpya maana zile za zamani, asilimia kubwa zimechakaa. Kumbuka hazijawahi kubadilishwa tangu ziwekwe miaka kumi iliyopita,” alisema Mwandumbya.

Kadhalika, alisema pia taa zilizopo kwenye ukumbi wa Bunge zitabadilishwa kutokana na nyingi kuungua na kufanya wapigapicha kukosa mwanga wa kutosha.

“Taa hazijawahi kubadilishwa maana kule juu zilipo ni mbali hivyo mkandarasi huyu ambaye amekuja kwa ujenzi wa paa na ukarabati mwingine, pia anabadilisha taa," alifafanua Mwandumbya.

Aidha alisema TBA ndiyo mshauri mwelekezi wa ujenzi wa jengo hilo.

Alibainisha ukarabati huo unafanya mmoja wa wakandarasi aliyeshiriki kujenga jengo hilo na kwamba fedha zinatolewa na Bunge.

Alisema ukarabati huo unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa Aprili, mwaka huu.

Habari Kubwa