Jeshi la Polisi laipongeza Taifa Gas kuwajengea vyoo

08May 2022
Na Mwandishi Wetu
KIGAMBONI
Nipashe Jumapili
Jeshi la Polisi laipongeza Taifa Gas kuwajengea vyoo

JESHI la Polisi limeipongeza Kampuni ya Taifa Gas kwa hatua ya kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyoo vya kisasa kwa ajili ya jeshi hilo eneo la Kigamboni Jijini Dar es Salaam. 

Katika hafla ya kupokea na kufungua rasmi vyoo iliyofanyika jana Kigamboni, Afisa Tawala wa wilaya, James Mkumbo ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Fatma Nyangasa, aliishukuru  Kampuni ya Taifa Gas ikiongozwa na Mkurugenzi wake Hamisi Ramadhani kwa ujenzi wa vyoo hivyo ambavyo vitasaidia pakubwa kuhakikisha jeshi hilo linafanya kazi katika mazingira yanayofaa. 

“ Vyoo hivi vipya ambavyo wanatukabidhi leo Taifa Gas ni ishara kwamba tuna majirani ambao wanatujali ni ishara kwamba tuna majirani ambao wanatambua kazi yetu katika jamii” alisema Mkumbo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba ya DC Fatma Nyangasa. 

Aliipongeza kampuni ya Taifa Gas kwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii huku akiitaja kampuni hiyo kuwa miongoni mwa kampuni chache nchini ambazo huwa tayari kushirikiana na jeshi la polisi nchini kwenye maendeleo. 

Meneja wa Operesheni wa Taifa Gas, Amos Jackson akisoma hotuba ya Mkurugenzi wa Taifa Gas Tanzania, Hamisi Ramadhani, alisema kuwa wametumia takribani  Shillingi million 32, kujenga vyoo sita, tatu kwa matumizi ya askari polisi wa kiume na tatu kwa ajili ya askari wa kike ambapo vyoo hivyo ni vya kisasa zikiwa pia na maeneo ya kubadilkishia nguo.

“ Huu ni mchango wetu na jukumu letu la corporate social responsibility kuhakikisha kwamba majirani wetu wananufaika na uwepo wetu katika jamii hii. Tutaendelea kutoa ushirikiano pale tutakapohitajika kwa ajili ya jamii” alisema 

 Alisema Taifa Gas imeendelea kuwekeza pakubwa katika kuhakikisha inatekeleza miradi mbalimbali katika jamii ambako kampuni hiyo imewekeza ikiwa ni utaratibu wao.

Kampuni ya Taifa Gas Tanzania LTD, wauzaji na wasambazaji wa gesi wa Taifa na Mihan gas nchini, leo wamekabidhi vyoo vilivyojengwa na kampuni hiyo, kwa ajili ya kusaidia jeshi la polisi Kigamboni. 

Habari Kubwa