Jeshi la Polisi latarajia kuteketeza silaha haramu zilizosalimishwa

21Nov 2022
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Jeshi la Polisi latarajia kuteketeza silaha haramu zilizosalimishwa

JESHI la Polisi nchini linatarajia kuendesha zoezi la uteketezaji wa silaha haramu ambazo zilisalimishwa katika kampeni maalumu iliyofanyika nchi nzima kuanzia Septemba Mosi, 2022 hadi Oktoba 31, 2022 iliyokuwa ikiongozwa na kaulimbiu isemayo “Silaha haramu sasa basi, salimisha kwa hiari”.

Taarifa hiyo imetolewa leo na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini SACP- David Misime ambapo amesema kampeni hiyo ilizinduliwa rasmi katika viwanja vya Mashujaa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, baada ya tangazo la serikali la msamaha wa usalimishaji silaha kwa hiari namba 537 lililotolewa Agosti 26, mwaka huu ambalo lilieleza kuwa yeyote anayemiliki silaha kinyume cha sheria anatakiwa kuisalimisha katika kipindi cha septemba Mosi hadi octoba 31, 2022, na yeyote atakayefanya hivyo hatashitakiwa.